Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack ametoa maelekezo hayo Jumamosi, tarehe 03 Juni 2023 akiwa mgeni rasmi kwenye kikao Maalum cha Baraza la Madiwani cha kupitia utekelezaji wa hoja za Halmashauri ya Mtama zilizoibuliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG kwa mwaka 2021/2022.
Kikao hicho ambacho kilifanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Mtama ambapo katika hoja zilizoibuliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2021/2022, ni pamoja na urejeshwaji mdogo wa fedha zilizokopeshwa Kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Mhe. Telack amewataka Maafisa maendeleo ya jamii kuwatafuta wanufaika wa Mikopo hiyo ambao hawajaresha na kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafikisha Mahakamani.
Ameongeza kuwa mikopo hii haitolewi na serikali kwa ajili ya Kula, kununua vitenge, kuchezea unyago au kuongeza mke. Fedha hizi zinatolewa mahususi Kwa ajili ya kufanya uzalishaji na biashara.
Mhe. Telack amesisitiza kuwa suala la nidhamu ya fedha lazima liwe kipaumbele kwa wakopaji vinginevyo watafungwa. Ameongeza kuwa Serikali haina nia ya kumfunga mtu lakini kama watu sio waadilifu hakuna namna.
"Sisi hatuna nia ya kufunga watu lakini unapokuwa mwizi unapelekwa wapi... Lazima tutoe mifano kwa baadhi ya watu....hakuna njia nyingine kama watu sio waadilifu sio waaminifu...wewe unachukua mkopo badala ya kufanyia biashara unaenda kuchangia harusi, kununua vitenge." Amesem Mhe. Telack.
Kwa upande wake, Muhasibu Mkuu wa Halmashauri ya Mtama Ndg. Sospeter Charles Urassa, akisoma taarifa ya hoja inayohusu kutolewa kwa Mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu pasipo kuzingatia uwiano wa 4:4:2 Kwa mwaka 2021/2022, amesema kuwa kasoro hiyo ilikwisha rekebishwa na Mikopo iliyotolewa kwa makundi hayo matatu imezingatia miongozo ya Serikali. Ameongeza kuwa kwa Mikopo iliyotolewa robo ya pili ya mwaka 2022/2023 imezingatia uwiano wa 4:4:2 ambapo vikundi vya wanawake wamepatiwa mkopo wenye jumla ya Tsh. Milioni 36, vikundi vya Vijana jumla ya Tsh. Milioni 36 na watu wenye ulemavu jumla ya Tsh. Milioni 18.
Akizungumza wa Waandishi wa Habari baada ya kikao, Mkaguzi Mkuu wa Mkoa wa Lindi ndg. Deogratius Patrick Mtenga amesema kuwa kikao hiki kinafanyika maalum Kwa ajili ya kupitia taarifa ya ukaguzi ya mwaka 2021/2022 kwa kuwashirikisha Madiwani, Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa.
Ndg. Deogratius ameongeza kuwa hoja zinazoibuliwa na CAG zinalenga kuboresha mifumo ya ndani ya Halmashauri na usimamizi mzuri wa sheria za fedha zinazotolewa na serikali kwa shughuli za Halmashauri ikiwemo miradi ya maendeleo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.