MHE. ZAMBI AMEAGIZA VIONGOZI NA WAJUMBE WA BODI YA NAHUKAHUKA AMCOS KUKAMATWA.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa, SACP. Renata Mzinga kuwakamata viongozi na wajumbe wa bodi ya Chama cha Msingi Nahukahuka kutokana na wizi wa fedha za wakulima wa korosho uliotokea tarehe 10/02/2017.
Viongozi wa AMCOS walikwenda kuchukua fedha benk kiasi cha shilingi 101,537,725 tarehe 10/02/2017 kwa ajili ya kuwalipa wakulima na baada ya kufika walilipa shilingi 29,576,492 tu kwa kuwa ilikuwa jioni na hivyo kuamua kuzifungia fedha nyingine ofisini.
Tarehe 10/02/2017 usiku fedha zilizokuwa zimebaki zenye jumla ya shilingi 71,961,233 ziliibiwa na hivyo kusababisha wakulima waliokuwa hawajalipwa kuanza kulalamika kwa kutokujua ni nini cha kufanya. Baada ya uongozi wa Mkoa na Wilaya kupata taarifa hizo, viongozi na bodi nzima ya Nahukahuka AMCOS walikamatwa na baada ya kufanya mahojiano nao ziliweza kurejeshwa fedha shilingi 56,000,000. Hii inaonyesha wazi kuwa viongozi wa chama cha msingi wamehusika na upotevu wa fedha hizi za wakulima.
Mhe. Zambi akiwa anaongea na wananchi na wanachama wa Nahukahuka AMCOS aliwauliza kama wanataka suala hili kulipeleka mahakamani au kama wanataka fedha hizi zilizopatikana wagawiwe kwanza wakati serikali ikiendelea kuwabana viongozi ili waweze rejesha fedha zilizobakia.
Kwa maamuzi ya pamoja ya wanachama na wananchi wa Nahukahuka walikubaliana kuwa fedha zilizopatikana kwanza wapewe ili ziweze kuwasaidia katika shughuli zao za maendeleo. Hivyo kutokana na maamuzi hayo ya wananchi Mhe. Zambi alimuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa kuwakamata viongozi wa AMCOS ili waweze kumaliza fedha zilizobaki.
“Viongozi wa vyama vya msingi wanatakiwa kuwa waadilifu na wanatakiwa kutambua kuwa kuchaguliwa kwao kunawafanya kuwa watumwa wa wanachama na wakulima na si vinginevyo”, alisema Mhe. Zambi. Pia aliwataka wananchi na wanachama wa AMCOS kuhakikisha wakati wa uchaguzi wa viongozi wawachague viongozi wenye sifa hasa katika uchaguzi ambao utafanyika mwaka huu.
Vilevile Mhe. Zambi alimuagiza Mrajisi Msaidizi wa Mkoa, Benjamin Mwangwala kuhakikisha anayafanyia kazi malalamiko ya wakulima kutopata viwatilifu kama ambavyo wameagiza kutokana na viongozi wa amcos kutokuwa waaminifu.
Aidha, Mhe. Zambi aliwaambia wakulima na wananchi kuwa ni muhimu kufungua akaunti kwani matatizo kama haya ya upotevu wa fedha yasingewapata kama wote wangekuwa na akaunti za benki.
Akimshukuru Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Shaibu Ndemanga alisema kuwa maamuzi ya Mkuu wa Mkoa kwenda Nahukahuka yamesaidia sana katika kuweka sawa uelewa wa jambo hili la wizi kwa wananchi. Pia aliwataka wananchi kuendelea kuwa pamoja na serikali na kutambua kuwa serikali inaendelea kuzifanya kazi changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Ndugu Mohamed Manzi alimshukuru Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya na viongozi wote waliokuwepo kwa kazi iliyofanyika mpaka kiasi cha fedha kupatikana. Kazi hii iliyofanyika imewafanya waongeze imani kubwa kwa serikali na hivyo kuahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa serikali.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.