Mhe. Zambi amewataka wanalindi kuwa na imani na serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi amewataka wananchi wa Mkoa wa Lindi kuwa na imani na serikali kwani serikali inaendelea kuzifanyia kazi kero mbalimbali walizonazo.
Mhe. Zambi alisema haya katika futari aliyokuwa ameiandaa kwa kushirikiana na Export Trading Group (ETG) iliyofanyika katika makazi ya Mkuu wa Mkoa. “Katika Manispaa ya Lindi zipo kero tatu kubwa ambazi ni tatizo la maji Umeme na kukosekana kwa kivuko cha Kitunda”, alisema Mhe. Zambi.
Serikali imekuwa ikiendelea kushughulikia kero hizi ambapo kwa sasa ujenzi wa mradi wa maji Ng’apa unakwenda kwa kasi nzuri na wataalamu wamehakikisha kuwa maji yatatoka tarehe 3 Julai, 2017 kama walivyomuahidi Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli alipotembelea mradi tarehe 3 Machi, 2017. Mradi huu wa maji unagharimu zaidi ya bilioni 29 na unajengwa na kampuni ya Overseas Infrastructure Alliance ya nchini India.
Kuhusu mradi wa umeme, aliwaeleza kuwa serikali inaendelea kumsimamia mkandarasi ambapo kwa sasa ujenzi unakwenda vizuri na mradi utakamilika mwezi Julai, 2017. Ujenzi huu wa mradi wa umeme unaojengwa na kampuni ya Electrical Transmission and Distribution Company (ETDCO) ya hapa nchini kwa gharama ya shilingi bilioni 16. Mpaka sasa ujenzi wa njia kubwa ya umeme kutoka Mtwara mpaka Maumbika kwenye kituo cha kupoozea umeme imekamilika hivyo wanaendelea kukamilisha kazi zilizobakia.
Aidha, Mhe. Zambi aliwaleza kuwa kazi ya ujenzi wa maegesho kwa ajili ya kivuko cha Kitunda unakwenda vizuri. Mkataba wa ujenzi huo unaishia Novemba, 2017 na utagharimu shilingi bilioni 1.9 ambapo Mkandarasi amemuhakikishia kuwa atakamilisha kazi wa wakati. Kivuko kitakachotumika tayari kimeshatengwa na serikali hivyo maengesho yakikamilika kitaletwa.
Pia aliwaeleza ETG kuhakikisha wananunua mazao ya wakulima kwa bei halali na sio kuwanyonya wakulima kwa kununua mazao kwa bei ya chini. Amewataka wao wenyewe kusimamia ununuzi badala ya kuwategemea watu wa kati ambao husababisha mkulima kunyonywa.
Vilevile aliwatakia waislamu wote funga njema katika siku zilizobaki huku akiwasihi kuendelea kuyaishi maisha mema hata baada ya mfungo wa Ramadhan kumalizika. Pia aliwaomba wananchi kuendelea kuwaombea viongozi na taifa kwa ujumla ili nchi iendelee kuwa na amani na utulivu.
Bi Fatma Ally ambaye ni meneja mahusiano toka EGT alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kukubali kushirikiana na nao katika kuandaa futari. “ETG imeamua kuungana na Mkoa na Wilaya kufuturisha ikiwa inaadhimisha miaka 50 ya uwepo wake” alisema Bi Fatma. Pia alisema kuwa ETG malengo yake ni kumuunganisha mkulima mdogo na soko la dunia, huku akisisitiza wakulima kuzalisha bidhaa zilizo na ubora kwani soko la dunia halina huruma kwa bidhaa mbovu.
Sheikh wa MKoa wa Lindi, Sheikh Mshangani aliwataka waumini kuwa kitu kimoja kwani sote ni binadamu hivyo tofauti za dini zisiwe sababu ya watu kugombana. Pia ameipongeza serikali kwa kazi nzuri zinazofanyika huku akiwasihi wananchi wote kuwaombea vingozi, serikali na taifa kwa ujumla.
Katika Futuru hii walishiriki viongozi mbalimbali wa taasisi za serikali na binafsi, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa wafanyabiashara, wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.