MHE. ZAMBI AWATAKA WANANCHI WA KIJIJI CHA MAKINDA KUTUNZA MIUNDOMBINU YA SHULE
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi amewataka wananchi wa Kijiji cha Makinda kilichopo katika Kata ya Mangirikiti Wilayani Liwale kutunza miundombinu ya shule ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Mhe. Zambi aliyesema hayo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi ambapo katika shule ya msingi Makinda aliweka jiwe la msingi ujenzi wa madarasa 6, vyoo viwili vyenye matundu 10 na madawati 150. Ujenzi huu unafanyika chini ya mradi wa Lipa Kulingana na Mtokeo (P4R) na umegharimu shilingi 141,000,000.
Kabla ya ujenzi wa madarasa haya, shule ilikuwa na madarasa 2, ofisi moja ya walimu na nyumba moja ya mwalimu. Shule hii ina jumla ya wanafunzi 230 na walimu 3. Baada ya kuweka jiwe la msingi, Mhe. Zambi aliongea na wananchi wa Kijiji cha Makinda waliokuwa wamekusanyika shuleni ili kushuhudia uwekwaji wa jiwe la msingi.
“Nianze kwa kuwapongeza kwa kazi nzuri ya ujenzi wa miundombinu ya shule uliyofanyika chini ya mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (P4R), niwasihi wanafunzi, walimu na wananchi wote kwa ujumla kuhakikisha mnaitunza na kuilinda miundombinu ya shule ili iweze kudumu kwa muda mrefu, alisema Mhe. Zambi.
Katika mkutano huo Mhe. Zambi alipokea kero toka kwa wananchi ambapo wananchi walizungumzia tatizo la maji, nyumba za walimu, upungufu wa walimu na kwamba kijiji hakina zahanati. Wakijibu kero za wananchi Mhandisi wa maji, Mhandisi Adrew Kilembe alieleza kuwa mwezi Septemba, 2017 kisima kirefu kitaanza kuchimbwa chini ya ufadhili wa Godrill Company.
Kwa upande wa upungufu wa walimu, Afisa Elimu Msingi Wilaya, Ndg. Joseph Mhagama alieleza kuwa Halmashauri tayari imeshaomba kibali cha ajira ya walimu na watumishi wa kada nyingine ambapo walimu hao wakiletwa walimu 5 watapelekwa shule ya msingi Makinda. Kuhusu upungufu wa nyumba za walimu alieleza kuwa katika fedha za mradi zitakazo letwa halmashauri imepanga kujenga nyumba moja ya mwalimu. Vilevile alieleza kuwa jamii nayo inabidi ishiriki kwa kuanza kujenga boma ili halmashauri ije kumalizia.
Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Maulid Majala alisema kuwa kijiji kinapata huduma ya afya katika zahanati ya jirani ya kijiji cha Kipule ambayo ipo umbali wa kilomita 4. Ila halmashauri imepanga kuingiza kwenye bajeti ya 2018/2019 ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Makinda.
Katika ziara hii, Mhe. Zambi alitembelea shule ya sekondari RM Kawawa, Likongowele ambapo amekagua kuona kazi zinazofanywa na walimu. Pia ametembelea zahanati ya Kijiji cha Mbonde ambapo wananchi aliowakuta walimueleza kuwa wanaridhika na huduma wanayopatiwa na watumishi wa afya katika zahanati.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.