Mhe. Zambi: Fanyeni kazi kwa uaminifu na uadilifu
Makatibu meneja wa vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) wametakiwa kuwa waaminifu na waadilifu katika kazi zao hasa kipindi hiki cha ununuzi wa korosho.
Wito huu umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi wakati akifunga kikao kazi cha makatibu meneja wa AMCOS ambacho kilifanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa.
Kikao hiki kilikuwa na lengo la kuwapa elimu ya pamoja juu ya namna mauzo ya korosho yatakavyoendeshwa msimu huu wa 2018/2019, namna bodi na mkoa ulivyojipanga, ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha majukumu yao. Pia mada mbalimbali ziliwasilishwa ambazo ni rushwa, bima ya afya, benki na watoa huduma za kifedha namna walivyojipanga, wakala wa vipimo, waendesha maghala pamoja na vyama vikuu.
Mhe. Zambi amewataka makatibu meneja kuhakikisha wanaelewa vizuri kuhusu bei dira na mjengeko wa bei. Ambapo amewataka kwanza waweze kutofautisha kwa kujua bei dira inapatikanaje na mjengeko wa bei unapatikanaje ili hata wakulima watakapokuwa wanawauliza waweze kutoa ufafanuzi mzuri.
“Kila mmoja wetu hapa amepata nakala ya mwongozo kutoka bodi ya korosho, hakikisheni mnakwenda kuusoma vizuri na mnatimiza yale yote yalimo ndani ya mwongozo huu”, alisema Mhe. Zambi. “Vilevile katika utendaji kazi wenu hakikisheni mnazingatia maelekezo yaliyotolewa wakati mada mbalimbali zikiwasilishwa”, aliongeza Mhe. Zambi.
Pia wametakiwa kuhakikisha korosho zote zinazoletwa na wakulima ni safi ili tatizo lililojitokeza mwaka jana kwa korosho kukutwa na mawe lisijirudie. Na kwa upande wa mizani wamesisitizwa kutohamisha mizani kuipeleka mashambani kwani kwa kufanya hivyo kunasababisha mizani kuharibika na kusababisha kipimo kutokuwa sahihi.
Naye mwenyekiti wa chama kikuu cha RUNALI, Hassan Mpako alisema kuwa kikao kama hiki ni muhimu sana kufanyika kabla ya msimu wa mauzo ya korosho kuanza kwani makatibu meneja wa AMCOS ndio waandishi na watunza kumbukumbu. Hivyo elimu na maelekezo waliyoyapata yatasaidia katika kupunguza au kuondoa kabisa mapungufu yaliyojitokeza katika msimu uliopita.
Aidha, katika kikoa hicho, makatibu meneja waliapa kiapo cha ahadi ya uadilifu katika kuvitumikia vyama vyao vya msingi mbele ya Mhe. Lilian Rugarabamu, hakimu mkazi mahakama ya mkoa wa Lindi, huku wakishuhudiwa na viongozi mbalimbali walioongozwa na Mhe. Zambi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.