Mhe. Zambi: Nendeni mkawe raia wema katika jamii
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi amewataka wafungwa 129 waliochiwa kwa msamaha wa Rais kwenda kuwa raia wema katika jamii.
Zambi ameyasema hayo wakati akizungumza na raia 34 waliokuwa wafungwa katika gereza la wilaya ya Lindi alipokwenda kushuhudia utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais Magufuli la kutolewa gerezani kwa wafungwa waliopata msamaha bila kuwekewa vikwazo vyovyote.
Raia hao wamewatakiwa kwenda kushirikiana na jamii vizuri katika shughuli za maendeleo, japo inaweza kukatokea changamoto ya kuchelewa kukubalika katika jamii kutokana na matendo waliyoyafanya. Hivyo amewasihi kuwa wavumilivu na watulivu kwa kuionyesha jamii kuwa muda waliokaa gerezani wamejifunza mambo mengi na wamebadilika kuwa raia wema wanaoaminika.
Zambi amewaeleza kuwa wanatakiwa kumshukuru Rais Magufuli kwa msamaha aliowapatia na endapo watarudia kufanya makosa ambayo yatawarudisha gerezani wajue hatua kali zitachukuliwa dhidi yao kwani itakuwa ni kuutumia msamaha wa Rais vibaya.
“Baada ya Mhe. Rais Magufuli kuwaachia kwa msamaha, ni mategemeo yetu kuwa mnakwenda kuwa raia wema na mkajiepusha sana na mambo ambayo yamewasababishia kufika gerezani”, alisema Zambi.
Naye Mkuu wa magereza mkoa wa Lindi, SACP. Josephine Semwenda amewasihi wanajamii kuwapa ushirikiano raia hao kwani wakiwa gerezani walipata fursa ya kujifunza shughuli mbalimbali zikiwemo za kilimo, ufugaji, ujenzi na nyinginezo. Aidha, amesema kitendo cha kuwanyanyapaa na kuwatenga kinaweza wasababishi raia hao kurejea kwenye kufanya matukio ya kihalifu na kufungwa tena gerezani.
Mmoja ya wafungwa walioachiwa huru, ndg. Juma L. Magayane amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia msamaha, na ameahidi kwenda uraiani kutenda matendo mema kwani amebadilika kitabia. Pia alisema kuwa amejifunza mambo mengi alipokuwa gerezani hivyo ni malengo yake kwenda kushirikiana na jamii katika shughuli za maendeleo.
Katika mkoa wa Lindi wameachiwa wafungwa 129 ambapo kati ya hao gereza la Lindi wapo 34, gereza la Kilwa wapo 24, gereza la Nachingwea wapo 20, gereza la Ruangwa wapo 29, gereza la Liwale wapo 9 na gereza la Kingulungundwa wapo 13.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.