Mhe. Zambi: Tumieni fedha za TASAF kujikwamua kiuchumi.
Wanufaika wa mradi wa TASAF watakiwa kutumia fedha wanazopata kujikwamua kiuchumi.
Haya yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi wakati akizungumza na wanufaika hao katika kijiji cha Songa mbele kilichopo wilayani Nachingwea ambapo alitumia nafasi hiyo kukagua miradi ya baadhi ya wanufaika.
Mhe. Zambi aliwaeleza wanufaika kuwa ni lazima watambue kuwa kuitwa maskini sio sifa hivyo ni lazima kila mmoja atumie fedha hizo katika kuwekeza kwenye miradi midogomidogo ambayo itamuwezesha kuendesha maisha yeke.
“Mradi huu wa TASAF hatuna uhakika kama utakuwa endelevu kwa miaka yote hivyo kila mnufaika anao wajibu wa kuhakikisha hizi fedha kidogo anazopata anazitumia kwa kuwekeza kwenye shughuli ndogo ndogo za kiuchumi kama ufugaji kuku lengo likiwa kujiongezea kipato”, alisema Mhe. Zambi.
“Lakini pia ni lazima uongozi wa wilaya upitie upya majina ya wanufaika kwani limekuwepo tatizo la kuchaguliwa watu ambao sio sahihi kutokana na vigezo vilivyowekwa, hivyo viongozi wa serikali ya kijiji ni lazima mhakikishe wale mnaowapendekeza wawe ni watu sahihi kwa mijibu wa vigezo vilivyowekwa”, aliongeza Mhe. Zambi.
Aidha, Mhe. Zambi wamewataka wataalam wa halmashauri kuhakikisha wanawatembelea mara kwa mara wanufaika wenye miradi kwa lengo la kuwapa ushauri wa kitaalam katika miradi wanayoitekeleza ili miradi hiyo iweze kuwa na tija.
Wanufaika wa mradi walieleza kuwa mradi huu umekuwa ni msaada mkubwa kwao kwani wengine umewawezesha kujenga/kumalizia nyumba, kuanzisha ufugaji wa kuku, kujiunga na vikundi vya kuweka na kukopa, hivyo wameishukuru serikali kwa kuwasaidia kupitia mradi wa TASAF.
Wilaya ya Nachingwea kwa kipindi cha Novemba – Decemba, 2018 imepokea kiasi cha shilingi 151,152,000 kwa ajili ya walengwa wa mradi wa TASAF ambapo walengwa wa Kijiji cha Songambele ambao ni kaya 51 wamepokea jumla ya shilingi 1,428,000.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.