Mhe. Zambi: Wadau tushirikiane kufanikisha zoezi la chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi
Wadau wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi Mkoa wa Lindi wametikiwa kutoa ushirikiano katika kuhakikisha zoezi hili la chanjo linafanikiwa pindi litakapoanza katika maeneo yao.
Haya yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi wakati akifungua kikao cha wadau wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Mhe. Zambi alisema kuwa lengo hasa la kuanzisha chanjo hii ni kuweza kuwakinga mabinti wenye umri wa miaka 14 dhidi ya madhara makubwa yanayoweza kuwapata kutokana na saratani hii ambayo husababisha vifo vingi kwa wanawake, chanjo ambayo itaanza kutolewa 23 April, 2018.
“Katika kipindi cha mwaka 2017/2018 jumla ya Wanawake 1720 waliweza kupimwa katika vituo vya kutolea huduma za Afya, kati yao waliogundulika viachanya (Dalili za awali za Saratani) ni 44 (2.6%). Waliopata huduma za awali (Cryotherapy) walikuani 44 (100%) na waliopata rufaa kwa ajili ya matibabu maalumu walikuwa ni 20 (1.2%)”, alisema Zambi.
Mhe. Zambi alisema kuwa mkoa kwa mwaka huu 2018 unatarajia kuchanja wasichana wasiopungua 14,905. Hivyo amewasihi wadau wote kwenda kuhamasisha jamii katika maeneo yao.
Aidha, aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanalisimamia zoezi hili kwa umakini na kuhakikisha fedha zinazoletwa kwa ajili ya kufanikisha zoezi hili zinatumika kama ilivyokusudiwa. Pia aliwaagiza waanze kuangalia namna ya kutenga fedha katika bajeti zao kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya zoezi hili kwa miaka ijayo.
Aidha, Mhe. Zambi ameishukuru Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na wadau mbalimbali waliochangia katika kufanikisha utoaji bora wa huduma za chanjo hapa nchini wakiwemo shirika la GAVI, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF), CHAI, JSI, PATH, AMREF, JHPIEGO pamoja na wadau wengine kwa misaada yao ambayo imeweza kutufikisha hapa.
Akizunguzia kuhusu baadhi ya vitu vinavyoweza kuchangia mtu kupata saratani hii, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Genchwele Makenge alisema kuwa ni pamoja na kuanza kujamiana katika umri mdogo, kuwa na wapenzi wengi, kuwa na ndoa za mitala, kuzaa watoto wengi na uvutaji wa sigara na kwamba dalili za saratani hii mara nyingi hujitokeza ikiwa imeshasambaa mwilini.
Hivyo ili kujikinga njia ya kwanza ni kupata chanjo ya kuzuia Saratani ya mlango wa kizazi, kutokufanya ngono katika umri mdogo, kuepuka kubeba mimba katika umri mdogo, kuwa na mwenzi mmoja mwaminifu, kutumia kondomu na kuepuka uvutaji wa sigara. Njiaya pili ni Kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini dalili za awali na kupata matibabu ustahiki mapema. Na njia ya tatu ni kupata matibabu maalum kwa mtu ambaye tayari amepata Saratani ya mlango wa kizazi.
Chanjo hii itatolewa katika utaratibu wa kawaida katika vituo vya kutolea huduma za Afya, baadhi ya shule zitakazochaguliwa, na baadhi ya maeneo katika jamii ambapo zitatolewa kwa njia za huduma za mkoba. Huduma hizi zitatolewa bila malipo katika vituo vya kutolea huduma za afya vya serikali na binafsi.
Elimu hii juu ya chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa Mkoa wa Lindi imetolewa kwa wadau mbalimbali wakiwemo Meya na Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Waganga Wakuu wa Wilaya, Maafisa Elimu Wilaya, Viongozi wa Dini, Waandishi wa Habari na wataalam wengine ambao wao ndio watakao kuwa wakilitekeleza zoezi hili.
Picha hapo chini zinaonyesha matukio mbalimbali wakati kikao kinafanyika ikiwa ni pamoja na uwasilishwaji wa mada mbalimbali kuhusu chanjo.
(Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.)
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.