Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amewataka wakandarasi waliokabidhiwa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya maji kufanya kazi zao kwa weredi na kuhakikisha kuwa wanakabidhi miradi hiyo kwa wakati uliopangwa ikiwa imekamilika.
Mhe. Telack ameyasema hayo wakati wa zoezi la utiaji saini wa mikataba ya miradi 15 ya ujenzi wa miundombinu ya maji yaliyofanyika baina ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na wakandarasi waliokabidhiwa miradi hiyo ambapo amesema “ Wakandarasi tunategemea kuwa mtatekeleza ujenzi wa miundombinu hii ya maji kwa wakati ambao tumepanga au chini ya wakati uliopangwa ikiwa imekamilika na tunaamini kuwa RUWASA wamefanya uchaguzi mzuri na wamewaamini hivyo msiwaangushe”
Aidha, Mkuu wa Mkoa amewataka RUWASA kuhakikisha kuwa wakandarasi wanalipwa stahiki zao mapema na kwa wakati ili kuwajengea mazingira mazuri wanapokuwa wanafanya kazi zao katika maeneo husika.
Katika taarifa yake, Meneja wa RUWASA Mkoa, Mhandisi. Muhibu Lubasa amesema hali ya upatikanaji wa maji maeneo ya vijijini katika mkoa wa Lindi umefikia asilimia 66.9 kwa mwaka 2021 na kuongeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo itaongeza upatikanaji wa maji safi na salama vijijini kwa asilimia 7.76 na kuongeza huduma ya maji kwa Mkoa wa Lindi hadi asilimia 74.66 kufikia Juni,2022.
“Katika utekelezaji wa shughuli za sekta ya maji katika mkoa wa Lindi, RUWASA leo inaingia katika mikataba kwa kusainishana na wakandarasi wa miradi ya maji 15. Jumla ya miradi 15 itakayosainiwa leo ina jumla ya fedha za kitanzania shilingi 7,100,605,415.22” Ameongeza Mhandishi. Lubasa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.