Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack Leo tarehe 26 Aprili 2023 amezindua ofisi mpya ya Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Lindi, iliyojengwa Mtaa wa Msinjahili, Manispaa ya Lindi.
Uzinduzi huo umefanyika kwenye Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanzania zilizofanyika nje ya ofisi hiyo zikihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Jeshi la Uhamiaji kutoka makao makuu na mikoa jirani, Viongozi wa Mkoa wa Lindi na Wilaya zake.
Akilipongeza Jeshi la Uhamiaji kwa kupata ofisi nzuri, Mhe. Telack amewaasa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Mkoa wa Lindi kuuenzi na kuutunza Muungano wa Tanzania kwa kuilinda amani ambayo ni tunda la waasisi wa muungano.
Mhe. Telack amewasihi wananchi wa Mkoa wa Lindi kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama pindi wanapoona viashiria vya uvunjifu wa amani ikiwemo kuwafichua waovu.
Kwa upande wake, Kamishna wa Jeshi la Uhamiaji Novaita Edmund Mroso Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi hilo nchini Tanzania amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kulipatia fedha Jeshi la Uhamiaji kwa ajili ya ujenzi wa Miradi mipya na kumalizia miradi ambayo ilikwama kwa muda mrefu ikiwemo jengo la ofisi za Uhamiaji Mkoa wa Lindi.
Kamishna Mroso ametoa shukrani kwa uongozi wa Mkoa na wananchi wa Lindi Kwa kufanikisha Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 59 ya Muungano wa Tanzania ambazo zimeenda sambamba na uzinduzi wa Jengo la ofisi ya Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Lindi.
Kamishna Mroso amesema kuwa jengo la ghorofa mbili lililozinduliwa kwenye Sherehe za Mkoa za Muungano wa Tanzania na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack lilianza kujengwa mwaka wa fedha 2012/13 ambalo limegharimu takribani Tsh. Bilioni 2.2.
Kamishna Mroso ameongeza kuwa kukamilika kwa jengo la Ofisi za Uhamiaji Mkoa wa Lindi ni hatua kubwa katika kufikia malengo ya miaka mingi ya kuwa na Ofisi ya Mkoa ambayo itawezesha utekelezaji wa majukumu kwa hari na ufanisi.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa, Mhe. Bakari Bwatamu ambaye ni Mwenyekiti wa Wilaya ya Lindi Mjini amesema kuwa Jeshi la Uhamiaji ni miongoni mwa majeshi yanayolinda amani ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Bwatamu ameendelea kwa kusema kuwa Jeshi la Uhamiaji ni walinzi wa mipaka ya kuingia nchini ambayo wamekuwa wakiilinda kwa uaminifu mkubwa.
Mhe. Bwatamu amewaasa Askari wa Jeshi la Uhamiaji ambao wanaelekea kustaafu wawaelekeze vijana wanaowaacha kazini mbinu wanazotumia kuilinda amani ya nchi kwa pande zote mbili za Tanzania bara na Zanzibar.
Mkoa wa Lindi Leo Jumatano imehitimisha wiki ya kilele cha Maadhimisho ya Muungano wa Tanzania ambapo katika Sherehe zilizofanyika, Mhe. Telack ametoa zawadi za ushindi kwa wanafunzi watatu walioshiriki kwenye shindano la kuandika Insha inayohusu Miaka 59 ya Muungano wa Tanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.