Katika kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika kimkoa Wilayani Liwale, waajiri wametakiwa kuhakikisha wanazingatia sheria, taratibu, miongozo na haki za wafanyakazi ili kujenga mazingira bora ya kazi.
Hayo yamesemwa na Mhe. Goodluck Mlinga, Mkuu wa Wilaya ya Liwale kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi alipokua akihutubia wafanyakazi, viongozi wa serikali, na wananchi waliohudhuria na kusisitiza kuwa uhusiano mwema baina ya waajiri na waajiriwa hauwezi kujengwa bila kufuata misingi ya haki, sheria za kazi na taratibu za ajira.
“Waajiri mnapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kuhakikisha mnazingatia sheria zote zinazohusu ajira. Haki ya mfanyakazi ni msingi wa maendeleo ya taasisi na taifa kwa ujumla,” alisema Mhe. Mlinga.
Aidha, amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuhakikisha sheria za kazi zinasimamiwa ipasavyo ili kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira salama, yenye staha na yenye kulinda utu wao.
"Waajiri wote wanapaswa kufuata sheria na miongozo ya kazi kwa kuzingatia sheria na maadili kazini namba. 366. Ninaagiza waajiri wote kuzingatia sheria hiyo na iwapo kuna malalamiko yapelekwe kwenye ofisi ya Kazi mkoa na kuyawasilisha malalamiko ya maslahi ya wafanyakazi katika mamlaka husika ili kuweza kuyafanyia kazi kwa wakati" ameongeza
Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu Ndg. Nathalis Linuma, akitoa salamu za Katibu Tawala Mkoa wa Lindi kwa wafanyakazi ameeleza kuwa ni muhimu kusheherekea sikukuu yao ya wafanyakazi na kuzingatia kauli mbiu inayohimiza ushiriki wa wafanyakazi katika Uchaguzi Mkuu na kuitafakari kwa kina ili kuitendea haki kwa wakati ili kuchagua viongozi ambao watatetea maslahi yao.
Nyabange Mgendi, Katiku wa CWT wilaya ya Nachingwea, ameiomba serikali kuendelea kutia mkazo kwenye maslahi ya wafanyakazi hususan katika stahiki zao ikiwemo mafao ya kustaafu, posho za likizo na uhamisho pamoja na kujiendeleza kimasomo.
“Tunashukuru serikali kwa kutambua mchango wetu, lakini pia tunaiomba iweke msisitizo kwa waajiri wote kuheshimu maslahi yetu na kupatikana kwa stahiki zetu pale inapotokea tumestaafu kama ilivyoainishwa kwenye sheria. Tuko tayari kufanya kazi kwa bidii, lakini tunahitaji mazingira rafiki na yenye usawa.”
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Mei Mosi 2025 inasema " Uchaguzi Mkuu 2025 Utuletee Viongozi Wanaojali Haki na Maslahi ya wafanyakazi , Sote Tushiriki "
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.