Mkoa wa Lindi jana tarehe 05 Juni 2023 umepokea mtambo wa kuchimba visima ikiwa ni katika jitihada za serikali kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji Safi na salama kwa jamii.
Akizindua mtambo huo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amesema kuwa ujio wa mtambo huu utasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto ya kina mama kuamka alfajiri kutafuta maji na badala yake watatumia muda wao vizuri kufanya shughuli za maendeleo.
Mhe. Telack amesema kuwa mtambo ulioletwa hauchimbi visima peke ake lakini pia una uwezo wa kutengeneza mabwawa yatakayosaidia kunyweshea mifugo.
Mhe. Telack ameitaka taasisi ya Bonde la Mto Ruvuma kufanya utafiti wa upatikanaji wa maji ya uhakika ili huduma ya maji ipatikane kwa wingi kwa kipindi chote cha mwaka mzima.
Aidha, Mhe. Telack amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ahadi yake toka alipokuwa Makamu wa Rais ya kumtua mama ndoo kichwani.
Mtambo huu wenye uwezo wa kuchimba visima 66 vyenye urefu wa mita 300 kwa mwaka umetolewa na Serikali kupitia fedha za UVIKO ambapo utaendeshwa na kusimamiwa na Wakala wa Usamabazaji Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini, RUWASA.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.