Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Kanali Ahmed Abasi amefanya kikao cha mapitio ya tathmini ya uboreshaji wa elimu katika mkoa wa Lindi pamoja na kuzindua mkakati wa kuboresha elimu msingi na sekondari katika mkoa wa Lindi ambao ulizinduliwa kitaifa na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 4 Agosti, 2022.
Akizungumza katika kikao hicho kilichowakutanisha wadau wa elimu pamoja na walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari katika mkoa wa Lindi, Kanali Abasi amesema kuwa mkakati huo umekuja muda mwafaka ambapo uboreshaji wa elimu msingi na sekondari unahitajika sana hivyo kawataka wasimamizi wote wa elimu kuhakikisha wanafunzi wote katika kila ngazi wanapata ujuzi, stadi na maarifa kama yalivyoelekezwa kwenye mihtasari ya mafunzo.
“Ninafahamu leo mtapitishana kwa karibu namna bora mtakavyokuwa mnatekeleza mikakati tuliyojiwekea katika kuhakikisha wanafunzi wanapata ujuzi unaotakiwa. Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi wote wanapomaliza darasa la kwanza wawe na stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu, wanafunzi wanapomaliza darasa la saba wawe na umahiri wa lugha ya kiingereza, wanafunzi wa ngazi za elimu ya msingi na sekondari kuwa na umahiri wa kila somo wanalofundishwa na walimu kwa ngazi husika” amesema.
Aidha, Kanali Abasi amewapongeza viongozi na wasimamizi wa elimu msingi na sekondari katika mkoa wa Lindi kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya katika kuboresha elimu na kuongeza ufaulu wa wanafunzi kwa ngazi ya mkoa na kuongeza “Ni matumaini yangu kuwa leo mtajipanga vizuri ili kuhakikisha mwaka huu 2023 tunaanza kivingine. Hakikisheni mnafanya tathmini kila mwezi na kujirekebisha kila inapobidi ili tutakapofika mwisho wa mwaka, sio tu wanafunzi wanafaulu bali pia wanafunzi wanakuwa na ujuzi na umahiri uliokusudiwa”
Mwalimu Suzan Nusu, Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Awali na Msingi amesema lengo la kikao hiki ni kukumbushana na kuweka mikakati ya kuboresha elimu msingi na sekondari kimkoa na nchini kiujumla ambapo pia ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama tawala kinachoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan.
“Ni matarajio yetu kuwa kikao kazi hiki kinaenda kuwajengea uwezo wa kutekeleza maagizo tunayoenda kupeana, lakini pia tunatarajia kikao hiki kuibua ari, kutiana shime na kupeana munkari wa kutekeleza majukumu, yan kila mmoja akitoka hapa ajue kuwa serikali inatambua mchango wake kila mmoja kwa nafasi yake, aidha tunazidi kuweka msisitizo katika matumizi ya vitabu vitatu vya miongozo ya elimu vilivyozinduliwa kwa lengo la kumpa mwalimu mwongozo wa ufundishaji”
Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Ndg. Ngusa Samike amesema katika mpango wa kuboresha sekta ya elimu mkoa umepokea jumla ya Tsh. 32,971,069,001.6 kutoka serikalini ikiwa na lengo la kupunguza tatzo la upungufu wa miundombinu ya madarasa, mazingira ya shule, madawati, meza, viti, nyumba za walimu, matundu ya vyoo, uendeshaji wa shule, ujenzi wa mabweni na ujenzi wa shule mpya.
“Kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 tulipokea Tsh. Billion 8,100,000,000 za kujenga madarasa 401 kwenye shule za sekondari na vituo shikizi. Katika program ya EP4R tumeletewa fedha Ths. Billioni 3,510,000,000 za ujenzi wa shule mpya 5 za msingi, vyumba vya madarasa 16, mabweni 10, mabwalo 4, maabara 5, nyumba za walimu 4 na ukarabati wa shule 1” ameongeza Katibu Tawala.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.