Mkurugenzi Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe- kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe akiongoza timu yake ya wakaguzi Jumamosi iliyopita wamefanya ziara ya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya ya Liwale.
Dkt. Ntuli ameongoza timu yake kufanya ukaguzi huo akiambatana na Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Khery Kagya na timu yake ya Mkoa pamoja na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Liwale Dkt. Groly Andrew na timu yake ya Wilaya.
Pamoja na ukaguzi huo, Dkt. Ntuli na timu yake walifanya ukaguzi wa huduma na utendaji kwenye Hospitali ya Wilaya ya Liwale na baadae jioni alifanya kikao na Viongozi wa Hospitali hiyo, Afisa Mfawidhi na baadhi ya watumishi wa Hospitali hiyo, Mganga Mkuu wa Wilaya na timu yake, Mganga Mkuu wa Mkoa na timu yake pamoja na wadau wanaotoa huduma za afya Wilayani hapo.
Akiongoza kikao hicho Dkt. Ntuli amesisitiza masuala ya uboreshaji wa miundombinu na huduma, kuimarishwa na usimamizi dhabiti wa vyanzo vya mapato, ushirikishwaji wa watumishi wote ikiwemo kusimamia stahiki zao pamoja na utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia miongozo iliyopo.
Katika kikao hicho, Dkt. Ntuli ameahidi kutatua changamoto mbalimbali ambapo Kwa kuanzia Serikali itapeleka magari mawili Hospitalini hapo pamoja na kutatua changamoto ya uchache wa watumishi kwa kuajiri watumishi kwa kuzingatia mazingira ya Wilaya ya Liwale.
Awali akizungumza mbele ya wajumbe wa kikao, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi Dkt. Khery Kagya akishukuru ujio wa Dkt. Ntuli na timu yake Mkoani Lindi, amesema kuwa ujio huo umesaidia kubainisha mapungufu katika maeneo mbali mbali ya Hospitali ya Wilaya ya Liwale huku akiahidi kufuatilia na kusimamia ipasavyo maelekezo yote yaliyotolewa kwa Mkoa mzima.
Dkt. Ntuli na timu yake wamefanya ziara Wilayani Liwale na Ruangwa Mkoani Lindi baada ya kufanya ziara kama hiyo Mkoani Mtwara. Ziara hii imefanyika maalum ikiwa na lengo kuu ka kuboresha huduma za afya zinazotolewa na Serikali Kwa jamii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.