Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack ametangaza oparesheni hiyo jana jumanne katika kikao chake na wafugaji wa mkoa wa Lindi kilichohudhuriwa na Viongozi wa CCM, Wakuu wa Wilaya, Mkuu wa Oparesheni na Mafunzo Tanzania, Kamati za Usalama za Mkoa na Wilaya, mwakilishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Wataalam wa mifugo.
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Telack ametangaza kupambana vikali na wafugaji walioingia kinyemela katika Wilaya za Lindi bila kufuata taratibu na kusababisha migogoro na wakulima.
Akizungumza kwa hisia kali, Mhe. Telack ameoneshwa kusikitishwa na vitendo viovu vinavyofanywa na wafugaji dhidi ya wakulima bila kujali utu wala hofu ya mungu.
“Kwenye ziara ya Waziri wa Mifugo, tulikuta watu zaidi ya saba wana vidonda vipya, wamekatwa vichwa, wameshonwa nyuzi mpaka kumi kwenye vichwa….ndugu zangu haiwezekani, Tanzania haiwezekani, hiyo Tanzania haipo…….. Wamama wanalalamika, yupo shambani amelima shamba lake anataka kwenda kuchuma mboga, mfugaji anamwambia chuma za leo tu halafu anaingiza mifugo kwenye shamba lake, halafu anamwambia mama kaa hapo ashuhudie anavyolisha mifugo kwenye shamba lake…haiwezekani.” Amesema.
Mhe. Telack amewataka wafugaji wote ambao hawana vibali mkoani Lindi waanze kuondoka mara moja kabla oparesheni ya kuwaondoa haijaanza. Pia amewataka wafugaji ambao wamekaa maeneo ambayo hawakupangiwa ikiwemo maeneo ya hifadhi za misitu waondoke mara moja huku akiwatahadharisha kuacha mapuuza.
“Nimesikia wakisema oparesheni wamezizoea, sasa oparesheni hizo ambazo zilifanyika na watu wengine sio hizi tutakazozifanya sasa…….watu wote ambao wameingia Lindi bila utaratibu ninasema nimetoa siku mbili tuanze kuswaga mifugo.”
Kwa upande wake Mkuu wa Oparesheni na Mafunzo Tanzania CP. Awadhi Juma akioneshwa kusikitishwa na vitendo vya kihalifu ikiwemo mauaji yanayofanywa na wafugaji, amesema jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vya kibabe vinavyofanywa na wafugaji dhidi ya wakulima na kuendelea kuhatarisha amani.
“ Mkoa wa Lindi kuna mauaji ya watu 12 ambao ni wakulima……na baadhi ya waliofanya uhalifu bado hawajakamatwa………… Sisi kama Jeshi la Polisi, chombo ambacho kimepewa dhamana ya kuulinda usalama wa raia na mali zao hatuwezi kukubali…………Wale ambao hawatatekeleza maelekezo na kuondoka kwa hiari yao, tutaendesha oparesheni kali mno hata kama hiyo mifugo ni ya kigogo wa namna gani tutahakikisha sheria inafuatwa.”
Kwa upande wao wafugaji wameeleza kuwa migogoro mingi inasababishwa na kukosekana kwa miundombinu ya maji kwenye maeneo mengi, uingiaji wa mifugo kwa njia za magendo lakini pia wizi wa mifugo. Akizungumza mbele ya kikao, Katibu wa wafugaji kanda ya Kusini Ndg. Daudi Balele amesema kuwa kwa kipindi hiki cha kiangazi maeneo mengi mashamba hayajalimwa, migogoro mingi inasababishwa na wezi wa mifugo. “ Nachingwea na Liwale ni Wilaya ambazo zina matatizo makubwa….kumezuka na wimbi la majizi ya mifugo ndio wanaogombana na wafugaji……………..unaanzaje kwenda kufyeka mifugo ambayo haina kosa…..kuna uvunjifu wa amani mkubwa mno.”
Oparesheni ya kuwaondoa wafugaji wavamizi mkoa wa Lindi inafanyika baada ya vitendo vya uvunjifu wa amani kati ya wakulima na wafugaji kushamili. Tangu kuingia kwa wafugaji mkoani Lindi kumeibuka migogoro inayosababisha mapigano kati ya wakulima na wafugaji ambayo yamekuwa yakigharimu maisha ya wananchi na wengine kujeruhiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.