Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amekemea vitendo vya rushwa katika utoaji wa huduma kwa wateja na maeneo ya kazi kwa ujumla.
Mhe. Telack amekemea vitendo hivyo viovu leo kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi la Mkoa wa Lindi kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Sea View. Akifungua kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe wa baraza hilo kutoka Wilaya za Lindi, Mhe. Telack amesema kuwa vitendo vya rushwa vinarudisha nyuma maendeleo ya taasisi na taifa zima. Ameongeza kuwa wafanyakazi wa Serikali wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na taratibu za utumishi wa umma ikiwemo upendo, kuheshimiana na kuepuka vitendo vya rushwa.
“Mambo ambayo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma hayapaswi ni pamoja na kutoa na kupokea rushwa, jambo hili linaturudisha nyuma sana, ukipokea rushwa ukiwa kwenye nafasi yako………..huwezi kufanya chochote kwake, umeuza utu wako, umeuza nafasi yako ya kazi, umeuza mamlaka ambayo umekabidhiwa.” Amesema Mhe. Telack.
Mhe. Telack amewataka wafanyakazi wa umma kuacha tabia zilizo kinyume na taratibu za kazi hasa rushwa ili kujenga jamii na taifa safi lisilo na rushwa.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi, Idara ya Utawala na Raslimali watu Dkt. Bora Haule amekemea wafanyakazi ambao hawazingatii maadili ya utumishi wa umma ikiwemo uvaaji mbaya, lugha mbaya, uchafu na unywaji pombe unaopelekea vitendo visivyofaa kwa jamii. Dkt. Bora pia amewataka wafanyakazi kutoa huduma bila upendeleo wa kundi lolote kama vile siasa, dini, undugu, urafiki na kusisitiza kuwa mfanyakazi ana wajibu wa kusimamia vizuri fedha na mali ya umma na ni wajibu wake kuzuia uharibifu, upotevu, ubadhilifu wa raslimali hizo.
Akisoma taarifa ya Baraza la Wafanyakazi, Katibu wa baraza hilo Mkoa wa Lindi ndg. Jumbe Kawambwa akiipongeza Serikali ya Rais. Samia Suluhu Hassan kwa kutatua changamoto nyingi za wafanyakazi wa serikali ikiwemo malipo ya malimbikizo ya madeni, upandaji wa vyeo, mishahara kutoka kwa wakati na mengine mengi ameahidi kufanya kazi kwa weledi, unyenyekevu na kujituma katika kuwasaidia wananchi na kufikia malengo ya Serikali.
Kikao cha Baraza la Wafanyakazi kimefanyika leo ili kujadili na kufanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 na mpaka kufikia Oktoba ya mwaka mpya 2022/2023.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.