Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack jumamosi ya tarehe 08 April 2023 amezindua Mpango Mkakati wa Elimu Kwa ajili ya maendeleo ya sekta hiyo Kwa mwaka 2023.
Mhe. Telack akizindua Mpango Mkakati huo kwenye mkutano uliofanyika katika kiwanja cha mpira cha Ilulu, Manispaa ya Lindi amesema kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Walimu wamefanya kazi kubwa ya kupandisha ufaulu wa wanafunzi kwa ngazi za msingi, kidato cha nne na kidato cha sita. Mhe. Telack ameongeza kuwa Kwa matokeo ya darasa la saba, ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 86.3 mpaka kufikia asilimia 86.42 na kushika nafasi ya nne kitaifa. Kwa kidato cha nne wanafunzi waliofaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu wameongezeka kutoka 2352 mwaka 2021 mpaka kufikia 2612 mwaka 2022. Kwa kidato cha sita , kwa kipindi cha miaka mitatu ufaulu umekuwa kwa asilimia 100.
Mhe. Telack amewapongeza Walimu, wazazi na wadau wote kwa ushirikiano mzuri uliozaa matunda hayo mazuri kwa Mkoa na Taifa Kwa ujumla.
Pamoja na maendeleo mazuri yaliyofikiwa kwenye sekta ya elimu, Mhe. Telack amewataka wazazi kushiriki kikamilifu kwenye utoaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni ili waweze kupata nguvu ya kuhudhuria masomo pamoja kuelewa wanachofundishwa darasani.
Ameongeza kuwa hali ya utoaji chakula shuleni bado hairidhishi ambapo Kwa Shule za Msingi utoaji wa chakula ni asilimia 60 Tu na upande wa Sekondari ni asilimia 80.
Katika kuhakikisha chakula kinapatikana kwa Shule zote, Mhe. Telack amezitaka Shule zote kuanzisha mashamba ya Shule ili kuzalisha mazao ya chakula.
Mhe. Telack ameongeza kuwa ili kufikia malengo yaliyowekwa kupitia Mpango Mkakati wa Mkoa, Walimu wahakikishe wanawafuatilia wanafunzi ili kujua changamoto zinazowasababisha washindwe kufikia malengo na kufanya vibaya kwenye masomo yao. Amesisitiza Walimu waendelee kusimamia nidhamu za wanafunzi ili kujenga kizazi Chenye maadili na kuweza kukabiliana na changamoto za mmomonyoko wa maadili Kwa wanafunzi na jamii nzima.
Mhe. Telack amewaasa Walimu kutizama adhabu za kuwapatia wanafunzi pale wanapokosea badala ya kuwafukuza Shule. Ameongeza kuwa kumfukuza Shule Mwanafunzi ni kumnyima haki yake ya msingi.
Awali akiwasilisha taarifa mbele ya mgeni rasmi, Afisa Elimu wa Mkoa wa Lindi Ndg. Joseph Mabeyo amesema kuwa Mpango Mkakati wa mwaka 2023 umeandaliwa kwa kuzingatia taratibu mbalimbali ikiwemo Sheria ya Elimu Na. 25 ya mwaka 1978 na marekebisho yake ya 10 ya mwaka 2002, Sera ya Elimu ya mwaka 2014, Nyaraka, miongozo na maelekezo ya Viongozi na Serikali.
Ndg. Mabeyo ameongeza kuwa Mpango Mkakati uliozinduliwa unalenga kutatua jumla ya changamoto 16 ikiwemo suala la utoaji wa chakula kwa wanafunzi pamoja na kusimamia maendeleo yao ikiwemo uwezo wa kusoma na kuandika kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga amewaomba Walimu kujipanga kikamilifu katika kuutekeleza Mpango Mkakati uliozinduliwa ili tofauti ionekane Kati ya Mkoa wa Lindi na mikoa mingine kupitia matokeo ya mitihani ya Taifa.
Aidha, pamoja na uzinduzi wa Mpango Mkakati wa maendeleo ya elimu, Mhe. Telack alitoa zawadi mbalimbali kwa wadau wote wa elimu walioshiriki katika kufanikisha matokeo mazuri ya mitihani ya taifa kwa ngazi zote za elimu kwa mwaka 2022.
ReplyForward |
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.