Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Mh. Ngusa Dismas Samike leo tarehe 16/8/2022 amesaini hati ya makubaliano ya mradi wa Mama na Mtoto Kwanza utakaosimamiwa na shirika la madaktari wasio na mipaka (MSF) ambao utafanyika katika wilaya ya Liwale, mkoani Lindi.
Awali, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi,Dokta. Kheri Kagya ameeleza kuwa mradi huo umelenga kuongeza na kuboresha huduma za mama na mtoto katika wilaya ya Liwale “Mradi huu unaenda kufanya kazi katika eneo la mama na mtoto ambapo tumekusudia kuboresha huduma za afya ya uzazi ili kupunguza vifo vya akinamama na watoto wachanga wakati wa kujifungua, tutapata wasaa wa kubadilishana na kupeana uzoefu yaani capacity building, lakini pia wafadhili wetu watatupatia nguvukazi watu ambapo tunategemea mradi huu utaajiri watumishi 41 ambao ili tu tuweze kuboresha huduma zetu na afya ya mama na mtoto na ndio msingi wa mradi huu wa Mama na Mtoto Kwanza”
Naye, Kiongozi wa MSF nchini ndg. Hassan Mieki amesema kuwa walifanya tafiti mbalimbali katika kubaini ni wilaya gani ina uhitaji zaidi wa huduma bora za mama na mtoto katika mkoa wa Lindi ambapo baada ya tafiti wakabaini kuwa uhitaji mkubwa upo katika wilaya ya liwale licha ya kuwepo kwa changamoto katika wilaya nyinginezo.
“Tunaamini ya kuwa mradi huu hautakuwa wa mwisho katika mkoa huu bado tutaendelea na miradi mingine kama njia ya kuona ni kwa namna gani tutaendelea kuboresha huduma za afya ili tuweze kusaidia jamii zetu katika sekta hii ya afya.” Ameongeza .
Aidha, mhe. Ngusa Samike, Katibu Tawala mkoa wa Lindi, amesema kuwa huduma za afya hasa afya ya mama na mtoto ni jambo ambalo halina mjadala na la umuhimu.
“Afya ya mama na mtoto ni jambo la umuhimu na halina mbadala, inasikitisha kuona mama anafariki wakati anajifungua hivyo inaleta faraja kuona na mashirika pia mnaunga mkono harakati za serikali katika kuboresha huduma hizi za afya, lakini pia tunavyofurahia kuletwa kwa miradi pia tujitahidi kuboresha, kusimamia huduma na utekelezaji wa miradi husika kwani tunaposhindwa kusimamia utekelezaji wa miradi hii kwa wakati tunakwamisha na kuchelewesha upatikanaji wa huduma za afya kwetu wenyewe na wananchi. Ameongeza.
Mradi wa Mama na Mtoto Kwanza unatarajiwa kutekelezwa katika zahanati 4, vituo vya afya 2 na hospitali ya wilaya 1 vyote ndani ya wilaya ya Liwale.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.