Mwenge wa Uhuru umepokelewa Mkoani Lindi leo tarehe 23 Agosti 2021 kutoka Mkoa wa Dar es salaam baada ya kumulika miradi mbalimbali ya Mkoa huo. Akiupokea Mwenge na timu ya wakimbiza Mwenge kitaifa wakiongozwa na Luteni. Josephine Mwambashi, Mhe. Zainab R. Telack amemueleza Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Amosi Makala kuwa Mwenge utakimbizwa takribani km 815.8 Mkoani Lindi kwa kudumisha amani, upendo na mshikamano ambapo utamulika miradi 42 mkoa mzima.
Kiongozi wa mbio za Mwenge Luteni. Josephine Mwambashi aliwaeleza viongozi wa Mkoa na Wilaya kuwa katika miradi yote inayomulikwa na Mwenge wahakikishe nyaraka na taarifa zote za mradi husika zinakuwepo eneo la mradi, wahusika wa mradi wawe na uwezo wa kujieleza na kujibu maswali. Pamoja na maelekezo hayo kiongozi huyo alisisitiza kuchukua hatua zote za kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19 ikiwemo uvaaji wa barakoa, kunawa kwa vitakasa mikono na kujitokeza kuchoma chanjo.
Aidha, baada ya makabidhiano ya Kimkoa, Mhe. Zainab R. Telack alimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Zainab Rashid Kawawa tayari kwa kuanza mbio hizo kumulika miradi ya Wilaya hiyo.
Baada ya kukabidhiwa Wilaya ya Kilwa, Mwenge ulifanikiwa kutembelea zaidi ya 11 ambayo ni mradi wa kituo cha afya Somanga pamoja na mifumo ya TEHAMA ya kituo hicho, mradi wa maji wa Somanga, Shamba la korosho ekari 50 la mkulima ndg. Hussein Yusuph, Klabu ya kupambana na rushwa na Klabu ya lishe za wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ilulu, mradi wa mashine ya kusaga ya watu wenye ulemavu kijiji cha Matandu, mradi wa kiwanda cha maji safi ya kunywa kilichopo Nangurukuru, mradi wa barabara ya kivinje yenye km 4.2, programu za mapambano dhidi ya malaria, madawa ya kulevya na UKIMWI Hospitali ya Kinyonga-Kilwa Kivinje na mwisho ni mradi wa usarishaji wa Kilwa jogging club.
Katika miradi yote iliyotembelewa na Mwenge, kiongozi wa mbio za Mwenge alikataa kuzindua mradi wa maji wa Somanga kutokana na kiasi cha fedha kilichotumia kutoakisi uhalisia wa mradi huo. Kiongozi huyo alisema “ mradi umekamilika lakini nyumba ndogo ya mtambo wa maji haiwezi kujengwa kwa Tsh. Milioni 26 na tenki milioni 150, hakuna uhalisia, fedha zimetumika nyingi ukilinganisha na mradi wenyewe.” Alisisitiza watendaji kutekeleza na kusimamia miradi kwa uzalendo na kisha aliagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi wa mradi huo.
Mwenge wa Uhuru unaendelea kukagua miradi ya Wilaya za Mkoa wa Lindi ukiwa na kauli mbiu “TEHAMA NI MSINGI WA TAIFA ENDELEVU; ITUMIE KWA USAHIHI NA UWAJIBIKAJI” ambapo utahitishwa na kukabidhiwa Mkoa wa Mtwara tarehe 28 Agosti 2021.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.