Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea ni miongoni mwa halmashauri katika Mkoa wa Lindi zinazonufaika na uwepo wa mradi wa BOOST wenye lengo la kuboresha utolewaji wa elimu ya awali na msingi.
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mhe. Mohamed H. Moyo ameeleza kuwa Wilaya ya Nachingwea pekee ilipokea kiasi cha Tsh. Milioni 931 na laki tano kwa ajiri ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule za msingi na awali.
''Wilaya ya Nachingwea tulipokea kiasi cha Tsh. milioni 931 na laki tano ambazo zimetumika kujenga madarasa 24, matundu ya vyo 34, shule mpya moja pamoja na jengo la utawala, kichomea taka pamoja na nyumba ya waalimu ambayo ni 2 in 1 na ujenzi wa madarasa ya awali ya mfano. Ujio wa mradi huu wa BOOST umepunguza sana changamoto ambayo ilikua inajitokeza kila ifikapo mwanzo wa muhula mpya wa masomo ambapo ilizoeleka sisi viongozi kukimbizana na wazazi kwa ajiri ya kupata michango ya kujenga madarasa ili tuweze kuendana na idadi ya wanafunzi walioandikishwa.'' Ameeleza Mhe. Moyo.
Aidha, Mhe. Moyo ameeleza kuwa ushirikishwaji wa wananchi katika utekelezaji wa mradi huu umesaidia sana kupatikana kwa matokeo chanya ''Kabla ya utekelezaji wa mradi huu wananchi walipewa elimu ili waweze kushiriki kwa karibu pamoja na kuunda kamati za ujenzi ambazo zilihusisha na wananchi pia, hii ilitusaidia sana kwani wanachi walishiriki kwa kujitolea nguvu zao katika ujenzi wa misingi ya majengo kwakua waliona kukamilika kwa mradi kwa wakati kutawaletea manufaa na afueni kwa watoto wao"
Bi. Neema Elias Sinane, Mwalimu wa Shule ya Msingi Tunduru ya Leo ameeleza shukrani zake kwa Serikali ya awamu ya 6 kwa kuleta Mradi wa BOOST uliofanikisha ujenzi na ukarabati wa majengo ya madarasa chakavu yaliyokuwepo awali katika shule hiyo.
''Huu mradi umetusaidia sana katika shule yetu, kama mnavyoona sisi tuna madarasa mengi chakavu hata watoto hususani wa darasa la kwanza na la pili katika usomaji kulikua na changamoto darasa ni dogo na watoto ni wengi hivyo hawasomi kwa nafasi, lakini ujio wa madarasa haya umetusaidia kwani watoto ambao walikua wanasoma katika madarasa chakavu sana wmehamia katika madarasa ambayo yana unafuu na hawa wadogo wamehamia katika madarasa mapya. Kwa sasa tendo la ufundishaji na ujifunzaji linafanyika kwa nafasi kwasababu ule mrundikano wa wanafunzi katika madarasa umepungua kwa kiasi kikubwa na kama jina la mradi lilivyo yaani BOOST umetuboost kwa namna yake hapa shuleni kwetu kwani sasa wanafunzi wanavutika kuja shule kutokana na miundmbinu mapya ya madarasa ilivyo'' ameeleza.
Bwana Lufungo Zebedayo, mzazi na mkazi wa kata ya Tunduru ya Leo ameeleza ni kwa namna gani wanajamii wameupokea na kushiriki katika utekelezaji wa mradi wa BOOST na namna unavyowanufaisha wanafunzi.
''Mimi kama mzazi nimefarijika sana kwa serikali hii chini ya Mama Samia kutuletea mradi huu kulingana na changamoto zilizokuwepo hususani ubovu na uchakavu wa majengo ya madarasa yaliyokuwa yanatumika na watoto wetu, majengo mengi kama yale yaliyopo pembezoni mwa barabara yote yalitakiwa yabomolewe yajengwe mengine, huu mradi umekuja kupuguza shida iliyokuwepo na tunaomba kama mradi huu ukiendelea basi tuletewe tena na hapa kwa maana kulikua na shida ya vyoo vya zamani lakini sasa vimepatikana vipya na wanafunzi wanafurahia vyo na madarasa mapya.
Vilevile, katika Shule ya Msingi Chiwindi iliyopo kata ya Chiwindi, Wilaya ya Nachingwea ambapo kulikua na changamoto kubwa ya watoto wa awali kusomea nje kwenye miti ya mikorosho kutokana na ukosefu wa miundombinu ya majengo hali iliyopolekea watoto wengi kukosa masomo ya elimu ya awali kutokana na utoro na mabadiliko ya hali ya hewa hususan mvua.
Mwalimu John Paul Nsumba, ameeleza ni kwa namna gani mradi wa BOOST umetatua changamoto hizo walizokuwa wanazipitia katika shule yao, ''Kupatikana kwa majengo haya kumeongeza chachu ya uandikishwaji wa watoto shuleni na uhudhuriaji wao darasani kwakua mwanzoni walikua wanasomea nje kwenye miti ya mikorosho hivyo wengi wao walikua hawafiki shuleni wanaishia tu majumbani,tulivyopata jengo hili la awali la mfano sasa uhudhuriaji wa wanafunzi umeongezeka, wanakaa darasani kwa nafasi na majengo yanavutia kutokana na uwepo wa picha, michoro na kona za ujifunzaji hivyo kuchochea ufanisi kwa wanafunzi na motisha za kujifunza kirahisi zaidi na kwa ushirikiano''
Kwa uhalisia mradi wa BOOST pekee hauwezi kumaliza tatizo la msongamano wa wanafunzi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wapya wanaoandikishwa kila mwaka kuanza elimu ya awali na msingi katika wilaya ya Nachingwea, na hapa Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea anaeleza ni kwa namna gani wilaya inaendelea kujipanga kukabiliana na changamoto hiyo.
''Kwanza kabisa tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi na tunawashukuru sana kwa nguvukazi wanazozitoa tunapokua katika utekelezaji wa miradi, lakini tunaendelea kuwahamasisha wananchi katika maeneo yetu kuanzisha benki za matofali ambazo zitaweza kutumika kwa kuanzia pale tutakapopata mahitaji kama kianzio katika ujenzi na pia tunaendelea kupokea michango mbalimbali kutoka kwa wadau mbalimbali kama hizi taasisi za kifedha hususan mabenki yamekua yanatushika mkono sana katika utatuaji wa changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sekta ya elimu kupitia misaada kama ya madawati na viti vinavyotumika na wanafunzi mashuleni"
Miradi yote ya BOOST inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea imeshakamilika na tayari imeshaanza kutumiwa na wanafunzi wa elimu ya awali na msingi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.