Nachingwea yapewa pongezi
Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea yapongezwa kwa kutoa mafunzo kwa vikundi kazi vya wanawake na vijana kuhusu utengenezaji wa barabara.
Akizungumza kabla ya kuwakabidhi vyeti wahitikimu wa mafunzo hayo Mkuu wa mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi ameupongeza uongozi wa wilaya ya Nachingwea na halmashauri kwa kuratibu mafunzo hayo. Pia amekipongeza chuo cha teknolojia stahiki ya nguvu kazi (ATTI) kwa kukubali kwenda Nachingwea na kutoa mafunzo kwa vikundi hivyo. Vilevile amewapongeza wanakikundi kwa utayari wao wa kupata mafunzo.
Zambi amewataka mameneja wa TARURA mkoa wa Lindi kuvitumia vikundi hivi hasa pale wanapokuwa na kazi ndogondogo za ukarabati na matengenezo ya barabara kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza ajira na uchumi kwa wananchi.
Wanavikundi wametakiwa kuhakikisha kazi watakazopata wanazifanya kwa weledi mkubwa na kutumia maarifa yote waliyopatiwa ili kuhakikisha ubora unaotakiwa unafikiwa. Zambi amesema iliyotengenezwa wakati wa mafunzo ni ya ubora sahihi ambayo mtu hawezikujua kama imetengenezwa kwa kutumia nguvu kazi na sio mitambo mikubwa.
Akizungumzia mafunzo hayo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Hassan Rugwa amesema halmashauri imetoa mikopo kwa vikundi kazi 15 ambavyo vimepatiwa mafunzo hayo na wakufunzi kutoka chuo cha teknolojia stahiki ya nguvu kazi (ATTI) kilichopo Tukuyu – Mbeya. Pia vipo vikundi 4 ambavyo vimejigharamia kushiriki kwenye mafunzo kutokana na kutokidhi vigezo vya kupata mkopo.
Vikundi hivi vimepatiwa mkopo wa milioni mbili kila kikundi ambazo zimetumika kugharamia mafunzo hayo na ununuzi wa vifaa anzia vya kazi (matoroli, masepetu, nyundo, sururu, majembe, shoka, tape measure pamoja na kufungulia ofisi zao za ukandarasi.
Rugwa ametaja faida ambazo vikundi hivyo vitazipata ikiwemo ya upataji ujuzi wa ukarabati na utengenezaji wa barabara kwa kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi, vikundi vinaweza kupata kazi za ukarabati na matengenezo ya barabara kupitia TARURA na TANROAD, na vikundi hivi vinakwenda kutambuliwa na bodi ya wakandarasi kwani vitapata vyeti vya BRELA na CRB.
Donata Amlima (mwanakikundi) ameishukuru halmashauri kwa kuwawezesha kupata mafunzo. Lakini ameiomba halmashari kuwasaidia kupata kazi hizo za barabara kwani hapo ndio watapata faida ya mafunzo na sio kuwategemea wakandarasi peke yake.
Naye Faki Chilumba (mwanakikundi) amesema licha ya kufanya kazi kwenye kampuni za ujenzi wa barabara, mafunzo hayo yamemjengea uwezo mkubwa kwani kuna mambo mengi ya kitaalam ambayo alikuwa hayajui. Pia elimu hiyo ataitumia katika kijiji chake pale watakapokuwa wanataka kutengeneza au kufungua barabara.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mhe. Ahamad Makoroganya amesema madiwani walitumia busara kubwa kubadilisha njia ya uwezeshaji vikundi ambayo ni ya kuvipatia elimu ya utaalam itakayo wapa ujuzi wa kufanya kazi badala ya kutoa kwa vikundi vya wajasiriamali peke yake. Halmashauri itakuwa ikivitumia vikundi hivi kwenye kazi za ufunguaji barabara.
Mkufunzi wa kutoka chuo cha ATTI, Mhandisi. Paul Henry amesema mafunzo hayo yanalenga kuviimarisha vikundi ili viweze kufanya kazi hizo katika ngazi za chini badala ya kuwategemea wakandarasi ambao huwa na gharama kubwa. Lakini pia hutolewa kwa wataalam wa ujenzi kutoka ngazi/idara mbalimbali zikiwemo TANROADS na TARURA.
Mhandisi. Henry amesema anaimani kuwa wahitimu wote watakwenda kufanya kazi kwa kuzingatia mafunzo waliyowapatia na itakuwa ni mwanzo wa barabara nyingi katika ngazi za vijiji na kata kufunguka.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.