Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea yaagizwa kuhakikisha mabanda yote ya biashara yaliyopo kwenye maeneo yake wanayamiliki.
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi alipokuwa kwenye ziara ya kikazi wilayani humo wakati akizungumzia suala la ukusanyaji wa mapato pamoja na uzibaji wa mianya ya upotevu wa mapato.
Zambi amesema halmashauri katika maeneo yake inayomabanda mengi sana lakini mapato yanayokusanywa ni kidogo kutokana na baadhi ya mabanda kuwa chini ya umiliki wa watu binafsi ambao hulipa sh. 5,000 kwa mwezi kwenye halmashauri. Katika mabanda ambayo halmashauri inayapangisha hutoza sh. 80,000 kwa mwezi.
Utofauti huo mkubwa wa kodi ya mwezi ndio uliomfanya mkuu wa mkoa Zambi kumuagiza mkurugenzi kuhakikisha mabanda yote hayo yanakuwa chini ya umiliki wa halmashauri.
“Hakikisheni yale mabanda yote ya biashara yaliyojengwa katika maeneo ya halmashauri mmnayamiliki na kwa maana hiyo mtatoza kodi ambayo ni stahiki ili kuongeza mapato,” alisema Mhe. Zambi.
Mkuu wa mkoa Zambi amesema hata kama kulikuwa na uzembe ulifanyika, sasa umefika wakati wa kuhakikisha taratibu zinazotakiwa zinafuatwa. Na katika utekelezaji wa hili kusijitokeze sababu zozote za kukwamisha utekelezaji wake.
Aidha, ameiagiza halmashauri hiyo kuhakikisha inakuwa na mpango wa kujenga au kuwa na mradi mkubwa unaotokana fedha za makusanyo ya mapato ya ndani badala ya kutegemea fedha za miradi kama hiyo kutoka serikali kuu.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hassan Rugwa amesema halmashauri imeshaanza kuvipitia upya vibanda vyote ikiwa ni pamoja na kuhakiki uhalali wa umiliki wake kwa wamiliki waliopo sasa. Hivyo amemuahidi mkuu wa mkoa kuwa atasimamia utekelezaji wa agizo alilolitoa na kuhakikisha vibanda hivyo vinakuwa chini ya umiliki wa halmashauri ili waweze kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Rugwa pia amesema halmashauri inaendelea na mkakati wa kubuni vyanzo vingine vya mapato na kuhakikisha inaboresha mazingira kwenye vyanzo vilivyopo lengo likiwa ni kuziba mianya ya mapato katika maeneo yote ya makusanyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.