Ngubiagai: Wananchi pandeni miti
Wananchi wametakiwa kupanda miti na kuitunza ili kusaidia utunzaji wa mazingira na kujiletea maendeleo.
Hayo yamesemwa na mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Christopher Ngubiagai wakati akizungumza na wananchi kwenye maadhimisho ya siku ya upandaji miti iliyofanyika kimkoa wilayani Kilwa.
Ngubiagai amesema wananchi wanao wajibu mkubwa wa kuhakikisha wanapanda miti ya aina mbalimbali katika maeneo yaliyotengwa kwa kazi hiyo ikiwa ni pamoja na upandaji wa miti ya matunda katika makazi yao.
Pia ameziagiza halmashauri kuhakikisha zinafanya mapitio ya hali ya miti iliyopandwa miaka ya nyuma ili kujua ni miti kiasi gani imekua, kwani kumekuwepo na tatizo la kutokuwa na ufuatiliaji wa ukuaji wa miti inayopandwa kila mwaka.
“Niziagize halmashauri zote katika mkoa wa Lindi kuhakikisha zinatenga maeneo kwa ajili ya upandaji miti na kupanda miti, pia kuhakikisha zinawahamasisha wananchi kupanda miti ya matunda katika maeneo yao”, alisema Ngubiagai.
Aidha, amewasihi wananchi kuendelea kutumia misitu katika kujiletea maendeleo kwa ufugaji nyuki na uvunaji endelevu wa misitu. Pia amezielekeza halmashauri kuendelea kuvisaidia vijiji ili viweze kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi ambapo itaviwezesha vijiji kuwa na mpango wa uvunaji endelevu wa misitu.
Akitoa salamu kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu, Dkt. Bora Haule alisema pamoja na kutenga maeneo ya kupanda miti ni vizuri pia kwa Halmashauri wakajiwekea utaratibu wa kuandaa kazu data ya miti iliyopo katika maeneo yao.
Awali akisoma taarifa ya miti ya mkoa Afisa Maliasili Mkoa, Zawadi Jilala alisema kuwa ili kuhakikisha shughuli za usimamizi shirikishi za misitu zinakuwa endelevu, Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii imeanzisha programu ya uongezaji wa thamani wa mazao ya misitu na nyuki unaofadhiliwa na serikali ya Finland.
Mkoa wa Lindi umeweka malengo ya kupanda miti mchanganyiko 15,000 kwa kila wilaya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.