Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Ndg Ngusa Samike amefanya ziara katika Halmashauri ya wilaya ya Mtama na kufanya ukaguzi katika mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi za Halmshauri ya Mtama ambao unatekelezwa na Mkandarasi wa Suma JKT kwa gharama ya TZS 3.77 Bilioni.
Utekelezaji wa mradi huo ulianza rasmi mwezi Novemba 2021 na ulitarajiwa kukamilika Novemba 2022 lakini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwa malipo ya mkandarasi cheti namba moja na mbili pamoja na kubomoka kwa msingi kwa kujaa maji kulikotokana na ucheleweshwaji wa kazi hivyo Halmashauri iliingia mkataba wa pili na Mhandisi Mshauri ambaye ni BICO kwa gharama ya TZS 154,000,000.
Katibu Tawala wa Mkoa amemtaka mkandarasi kukamilisha mradi huo katika miezi sita ya nyongeza aliyopewa "Serikali imejitahidi kuleta fedha ili kuwasaidia watumishi kupata ofisi nzuri zitakazowasaidia kutoa huduma kwa wananchi kwa urahisi na kuwapunguzia lakini pia itasaidia kupunguza usumbufu na adha kwa wananchi kutembea umbali mrefu wanapowahitaji wataalamu ambao kwa sasa wapo maeneo tofauti tofauti, niwatake sasa kwa muda wa miezi sita ambao mumeomba kuongezewa mjitahidi na kuongeza nguvu kazi hawa watu waliopo hapa site hawatoshi na hatuwezi kufikia lengo hapa tusidanganyane"
Aidha, Katibu Tawala wa Mkoa amesisita ubora na uimara wa majengo kulingana na thamani ya fedha inayotumika pamoja na utumiaji wa rasilimali ambazo zinapatikana ndani ya Halmashauri kiurahisi ili kufikia malengo ya miradi na pia kupunguza matumizi ya fedha yasiyo na ulazima ili fedha hiyo iweze kutumika katika miradi mingine ya maendeleo ndani ya Halmashauri.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama Ndg. George Mbilinyi amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi huo utasaidia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi wa Mtama pamoja na usimamizi wa watumishi wanapokuwa katika majukumu yao ya kazi.
"Tunapoenda kukamilisha huu mradi maana yake tunaenda kuwarahisisha wananchi kupata huduma katika eneo moja, kuliko sasa hivi mwananchi anaweza kutembea hadi kilometa 4 kutoka ofisi ya Mkurugenzi kufata huduma katika idara nyingine kama maendeleo ya jamii lakini pia itanirahisisha hata mimi kufuatilia utendaji kazi wa watendaji wangu katika halmshauri kwasababu kwa sasa muda mwingine inaniwia vigumu kumfatilia mtumishi ambaye ofisi yake ipo kilometa 4 kutoka hapa kujua kama amefika ofisini au la"Amesema.
Halmashauri ya wilaya ya Mtama ni moja ya miongoni mwa Halmashauri zilizokuwa hazina majengo ya Utawala, hivyo kutokana na kuwepo kwa adha hiyo ya kukosekana kwa ofisi serikali iliona umuhimu wa kujengwa kwa jengo la ofisi za Halmshauri.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.