Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Ndg. Ngusa Samike amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zilizopo katika Mkoa wa Lindi kusimamia vizuri miradi wanayoletewa ikiwemo kuhakikisha fedha za miradi husika haziishi kabla ya miradi hiyo kukamilika.
Katibu Tawala ameyasema hayo alipokua katika ziara yake wilayani Kilwa ambapo ameshangazwa na hali ya kutokukamilika kwa miradi ya elimu huku changamoto kubwa ikiwa ni kumalizika kwa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi wa Shule ya Sekondari Somanga Bwana Ezekiel Mulula, mwalimu wa shule ya sekondari Kinjumbi amesema “ Mnamo tarehe 24 Novemba 2021 tulipokea kupitia akaunti ya shule kiasi cha Tshs. Milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari katika kata ya Somanga ambapo mradi unahusisha ujenzi wa madarasa manane, maabara tatu, jengo la utawala, maktaba, jengo la kompyuta, matundu 20 ya vyoo pamoja na mfumo wa maji.”
Aidha, Bwana Mulula ameongeza kuwa kutokana na gharama za vifaa vya ujenzi kuongezeka wanaomba kuongezewa fedha kwa ajiri ya kuhakikisha mradi unakamilika kwa asilimia 100%.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Katibu Tawala amesema “Mkurugenzi na timu yako mufanye tathmini ya kiasi gani kinachotakiwa katika kukamilisha mradi huu kisha uje na mkakati wa namna gani hiyo fedha itapatikana ikiwemo na uwekaji wa madawati ili ifikapo mwezi Oktoba mradi uwe ushakamilika na watoto waanze kusoma hapa”
“Jukumu la mkoa na watumishi wengine wakiwemo watendaji wa kijiji wote wana wajibu wa kukagua miradi na kuhakikisha thamani ya fedha iliyotolewa inaendana na kazi inayofanywa hii inaenda sambamba na kuhakikisha mafundi hawakai maeneo ya ujenzi kwa muda mrefu bila kufanya kazi yoyote hii itapunguza gharama tunazotumia katika kuwalipa, inasikitisha kuona fedha ya mradi inaisha na mradi haujakamilika tunaanza kuomba fedha nyingine wakati maeneo mengine wametumia fedha hizohizo na wamekamilisha, sisi huku tunashindwa wapi?” ameongeza Katibu Tawala.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.