Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na Redio Uhuru fm wameandaa mbio za hiari ambazo zinafahamika kama uhuru sensa marathon ambazo zinatarajiwa kufanyika tarehe 13 mwezi huu katika viwanja vya majengo vilivyopo katika Halmashauri ya Mtama, Mkoani Lindi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jumatatu kuhusu mbio hizo Katibu Tawala mpya wa Mkoa wa Lindi Ndugu Ngusa Samike amesema kuwa mbio hizo zinalenga kuhamasisha wananchi pamoja na kuunga mkono zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika agosti 23 mwaka huu.
Mheshimiwa Ngusa amewakaribisha wananchi na wadau mbalimbali katika kushiriki mbio hizo huku akisisitiza kuwa kushiriki mbio hizo itakuwa ni chachu kwa wananchi katika kushiriki zoezi la sensa hapo baadae.
Naye mratibu wa mbio hizo Dkt. Bora Haule amesema kuwa mpaka sasa hamasa ni kubwa na tayari baadhi ya washiriki wameanza kujiandikisha na pia amewataka wananchi wa Lindi kujitokeza kuhesabiwa katika siku ya sensa.
Mbio hizo zinatarijwa kushirikisha wakimbiaji wa kilomita tano na kilomita kumi, huku zawadi kadhaa zikitolewa, kwa upande wa washindi wa kwanza upande wa wanawake na wanaume wao watajinyakulia zawadi ya shilingi 500,000 huku washindi wa pili kwa jinsia zote watapewa shilingi 300,000 na washindi wa tatu nao watapewa zawadi ya shilingi 200,000 kila mmoja.
Aidha mbio hizo zitawahusisha pia washiriki wenye ulemavu huku baadhi yao wakiwa tayari wameanza kujiandikisha kushiriki mbio hizo.
Akiongezea kuhusu ushiriki wa mbio hizo Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Uhuru fm Bi. Amina Azizi alisema kuwa kujiandikisha kushiriki mbio hizo ni bure na amewaomba wananchi wa Lindi wajitokeze kwa wingi kushiriki mbio hizo na kuhamasisha zoezi la sensa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.