Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa wametakiwa kuacha visingizio na badala yake waongeze kasi ya usimamizi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hasa za afya kwa wananchi.
Maagizo hayo yametolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Ngusa Samike wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya afya na elimu katika wilaya ya Kilwa ambapo amebaini uzembe unaofanyika na watumishi hao katika usimamizi wa mradi wa ujenzi wa kituo cha afya uliopo katika kijiji cha Kipindimbi.
Akitoa taarifa ya mradi bi. Emiliana Mlelwa, mganga mfawidhi wa zahanati ya Kipindimbi amesema “Mradi wa kituo cha afya Kipindimbi unagharimu kiasi cha shilingi Milioni 500,na ulichelewa kutekelezwa kutokana na mgogoro ulioibuka katika kijiji cha Njinjo kwa kudai kuwa kituo kinapaswa kujengwa Njinjo badala ya Kipindimbi, hivyo mradi ulianza kutekelezwa tarehe 16/01/2021 baada ya kupokea maelekezo kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa na ulitarajiwa kukamilika tarehe 17/04/2022, lakini pia tumekuwa na changamoto ya kufungwa kwa mfumo wa malipo na kupelekea mafundi kutokuwepo site pamoja na wazabuni kuchelewesha vifaa”
Katika kuhakikisha mradi huo unakamilika Katibu Tawala amewataka wasimamizi wa ujenzi huo kuacha visingizio na kuhakikisha mradi huo unakamilika “wasimamizi wa huu mradi hasa ambao ni watumishi tuache visingizio kama vile uwepo wa mvua au kufungwa kwa mfumo wa malipo kama sababu ya mradi kutokukamilika, tukubali tu kuwa kuna uzembe katika usimamizi,naagiza mradi kuendelea na ujenzi kuanzia kesho, mkurugenzi naomba uhakikishe mafundi wanakua site huku taratibu za kukagua thamani za mradi zikifuata”
Aidha, amemtaka mganga mkuu wa wilaya ya kilwa kuanza taratibu za kuomba watumishi, madawa na vifaa tiba ili punde mradi utakapokamilika uanze kutoa huduma kwa wananchi.
Mradi wa kituo cha afya Kipindimbi unajumuisha majengo matano ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la maabara, jengo la kufulia, jengo la upasuaji na jengo la wodi ya wazazi, pia unatarajiwa kuhudumia wananchi wapatao 30,861 wa kata ya Njinjo pamoja na wakazi wa kata jirani za Miguruwe, Kandawale na Mitole.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.