Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zainab Telack amezindua kampeni ya utoaji wa chanjo ya ugonjwa wa Polio kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka 5, inayotarajiwa kufanyika katika mkoa wa Lindi kuanzia Aprili 24 hadi Mei 1.
Katika kikao hiko Mkuu wa Mkoa amewaomba viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini kutoa hamasa kwa waumini wao (wananchi) ili kuwafanya washiriki kikamilifu katika zoezi hili la utoaji wa chanjo kwa watoto ambalo linatarajiwa kufanyika nyumba hadi nyumba ili kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo hiyo.
“Niwatake wahudumu wa afya tuwe na umoja na ushirikiano katika kulitekeleza zoezi hili la utoaji wa chanjo ya polio kwa watoto wetu, tukawe rahimu, tukawe na upendo katika kuwahudumia na kutoa chanjo kwa watoto wetu hawa” ameongeza Mhe. Telack.
Aidha, utoaji wa chanjo ya Polio unatarajiwa kuwafikia watoto wapatao 156,605 ndani ya mkoa wa Lindi ambapo Wakurugenzi na Maafisa wa Afya katika kila Halmashauri wametakiwa kuhakikisha kuwa fedha za chanjo zinatolewa kwa 100%.
Pia, katika uzinduzi huo Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi kwa kuyafanyia usafi na kufyeka nyasi ili kuharibu mazalia ya wadudu waenezao maradhi kama Mbu.
“Muwaambie watu wafyeke nyasi katika maeneo yao hasa katika msimu huu wa mvua, na sio kupulizia dawa mkawaambie madhara ya kupulizia dawa za kuua nyasi kuzunguka nyumba zao alafu wakaingia ndani kulala na watoto wao, wapeni elimu hawa wananchi na iwe marufuku kupulizia dawa hizi zenye sumu. Usafi kwenye barabara zetu na mitaro inayozunguka maeneo yetu isafishwe na hiyo kazi ifanyike kila Jumamosi katika wilaya zetu zote. Tunataka mashindano ya usafi kwa mikoa na sisi Lindi tuwepo na tuwe namba moja” Mhe. Telack.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.