Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amewataka Waganga Wakuu wa Hospitali za Wilaya kutoa elimu ya lishe kwa jamii ili kupata kizazi chenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi. Mhe. Telack ameyasema hayo kwenye kikao cha kusaini mikataba ya utekelezaji masuala ya lishe kati ya Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika jumanne katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa na kuhudhuriwa na Kamati za Usalama, kamati za lishe za Mkoa, Wilaya pamoja na wafadhili wakuu Save The Children, Mhe. Telack akisisitiza utoaji wa elimu amesema kuwa lishe duni ndiyo chanzo cha matatizo yanayotokea kwenye jamii ikiwemo kupigana hovyo.
“Sote tunajua kwamba tukisimamia lishe tutakuwa na watu wenye maamuzi…sio tunazaa watoto wanapiga wenzao mikuki……ukiangalia utakuta kuna matatizo kwenye kichwa…….tusaidiane kujenga nchi yetu, tusaidiane kujenga watoto wetu.”
“Elimu ya lishe itolewe kwenye vituo vyote vya kutolea huduma kabla kina mama hawajapima ujauzito, lakini kabla watoto hawajapimwa, wazazi wanahitaji kupatiwa elimu….mwingine anampa mtoto wake kile anachokiona na hajui madhara yake ili mradi mtoto ashibe, sasa wataalam tusaidieni…..kwenye vituo vya afya tukawe na orodha ya vyakula vya lishe bora…..wazazi wafundishwe.”
Kwa upande wake Mratibu wa Lishe Mkoa wa Lindi Ndg. Lewis Mahembe amesema kuwa kwa sasa Mkoa wa Lindi unapiga hatua nzuri kwenye uboreshaji wa lishe kwa jamii ambapo kwa takwimu za mwaka jana Mkoa wa Lindi ulikuwa wa tatu kutoka mwisho na mwaka huu mkoa umeshika namba 10 kitaifa. Ndg. Lewis ameongeza kuwa changamoto kubwa kwenye utekelezaji mpango wa lishe ni matumizi ya fedha zilizopangwa kuboresha lishe kutumika kinyume na mpango huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Ndg. Ngusa Samike amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Lindi kutumia fedha za lishe kama inavyoelekezwa na Serikali ili kufikia malengo yaliokusudiwa. Ndg. Ngusa pia amewataka Waganga Wakuu wa Wilaya pamoja na Maafisa Lishe kuwajibika ipasavyo katika kuboresha afya ya mama na mtoto.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.