Wakala wa Nishati ya umeme Vijijini REA imeweka mpango wa usambazaji umeme kwa vijiji 37 ambavyo bado havijapata huduma hiyo. Kati ya vijiji 74 vilivyopo Wilaya ya Liwale ni vijiji 39 ndio vilivyofikiwa na huduma ya umeme wa REA.
Hayo yamebainika Leo katika kijiji cha kichonda, Wilayani Liwale muda mfupi baada ya Mwenge wa Uhuru kuwasili kijijini hapo kwa ajili ya kutembelea na kuona ujenzi wa laini ya msongo wa kati, msongo mdogo, ufungaji wa mashine umba pamoja na uunganishaji wa wateja wa umeme katika kijiji cha Kichonda.
Akiwasilisha taarifa ya usambazaji umeme wa REA kwa niaba ya Meneja wa TANESCO mbele ya Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru, Mhandisi Benson Mbigili amesema kuwa vijiji 37 ambavyo havijafikiwa na huduma ya umeme tayari Vimeingizwa kwenye mpango wa usambazaji umeme Vijijini awamu ya tatu mzunguko wa Pili.
Mhandisi Mbigili ameongeza kuwa kupitia Mpango huo utakaomalizika tarehe 30 Aprili 2023 chini ya Mkandarasi White City Guangdong , vijiji vyote 74 vya Wilaya ya Liwale vitasambaziwa huduma ya umeme.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndg. Abdalla Shaib Kaim ametoa pongezi zake kwa kazi kubwa ambayo inafanywa na TANESCO huku akisisitiza vijiji vyote visambaziwe huduma ya umeme kwa wakati.
Mbunge wa Liwale, Mhe. Zuberi Kuchauka ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha huduma mbalimbali za wananchi ikiwemo kuwasambazia huduma ya umeme.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.