Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi wamefanya kikao na wadau leo tarehe 27 Januari, 2023 chenye lengo la kujadili maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya REA kwa awamu ya Tatu mzunguko wa Pili katika mkoa wa Lindi ambao umeganywa kwa wakandarasi wawili, Nakuroi Investment Company Limited (Lot 10) na White City International Contractors LTD (Lot 11).
Mhandisi Thomas Mbaga, Kaimu Mkurugenzi Mkuu REA ameeleza kuwa mradi wa REA awamu ya Tatu, mzunguko wa Pili kwa mkoa wa Lindi unagharimu kiasi cha shilingi za kitanzania Bilioni 71.915 na unatekelezwa katika wilaya za Kilwa, Lindi Vijijini (Mtama), Ruangwa, Nachingwea na Liwale ambapo mikataba yake ilisainiwa mnamo Juni 2021 na kutegemewa kukamilika ndani ya muda wa miezi 18.
“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote vilivyopo Tanzania Bara vinafikiwa na miundimbinu ya umeme, na huu ndo mradi wa kufunga mambo yote ya kupeleka umeme katika vijiji vyote vya Tanzania Bara. Katika mkoa wa Lindi vijiji 198 vipo katika utekelezaji wa mradi wa mradi huu wa REA Three, Phase two ambapo Nakuroi Investment yeye anapeleka umeme katika vijiji 92 vya wilaya ya Kilwa, Lindi vijijini pamoja na Ruangwa. Na Mkandarasi White City anapeleka umeme katika vijiji 107 ambavyo vipo katika wilaya za Nachingwea(70) na Liwale(37)”
Mhandisi Mbaga ameongeza kuwa katika utekelezaji wa mradi huo katika maeneo mbalimbali kumejitokeza changamoto kadha wa kadha ambazo zimechochea kudhorotesha ufanisi wa utekelezaji wa mradi huo katika maeneo ya miradi
“Kulitokea na ongezeko ambalo si la kawaida la vifaa ikiwemo nyaya kwahoiyo ongezeko hilo lilisababisha tukae chini na kujadili ni kwa namna gani tunaweza kulitatua na tunashukuru tumeweza kulipatia utatuzi na tumeshaona ni sehemu gani tunaweza kuboost ili zoezi hili lisikwame, lakini pia tulipata changamoto za wizi wa vifaa na uwepo wa baadhi ya vijiji katika Pori la Akiba la Selous hivyo kuhitajika vibali vya serikali ili kuemdelea na shughuli hizo”
Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Ndg. Ngusa Samike amewataka wakandarasi kuacha visingizio na kujitahidi kumaliza kazi kwa wakati uliowekwa ili kuisahidia serikali kufikisha huduma kwa wakati sahihi kwa wananchi na kwa ubora unaotakiwa.
“Wakandarasi mnaofanya kazi kwatika miradi iliyopo hapa Lindi tunawataka muache visingizio, mliomba kazi, mkapewa kazi, mkafanye kazi ndo ujumbe tunawapatia, na kwakua mumekuja na mnalipwa fedha za serikali ni vyema mkaenda kufanya kazi kwa mujibu wa mkataba kwanza mtekeleze mradi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.nikifika maeneo ya mradi nategemea kumuuliza swali mkandarasi na anijibu kwa kueleweka kwasababu matarajio yrtu sisi ni wananchi wa mkoa wa Lindi wapate huduma inayostahili”
Kwa upande wa wakandarasi wameeleza kuwa mfumuko wa bei za vifaa hasa zenye asili ya chuma ndizo zilizochochea wao kushindwa kukamilisha miradi yao kwa wakati uliopangwa.
“Hadi sasa hivi tunaendelea vizuri, tulikua na baadhi ya changamoto hasa ya kuongezeka kwa bei za vifaa vyenye asili ya chuma kama nyaya bei ilipanda ikawa kubwa kubwa sana tunaishukuru serikali iliingilia kati na kutusaidia kutatua changamoto hiyo, na hivyo tunaamini katika miezi hii mitatu iliyobaki tunaweza kukamilisha kabisa kazi tulizokuwa nazo” Mhandisi Jacqueline Mushi, Meneja Miradi wa kampuni ya White City.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.