Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais. Mhe. Samia Suluhu Hassan imetoa pembejeo za uzalishaji wa zao la korosho kwa wakulima wa zao hilo. Pembejeo hizo zinatolewa kwa wakulima kuanzia tarehe 16 Mei 2022.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Ndg. Kelvin Mwaisomi akizungumza kwenye kikao cha tathmini ya ununuzi wa korosho msimu wa 2021 na maandalizi ya msimu wa ununuzi wa ufuta 2022 kilichofanyika alhamisi ya tarehe 12 Mei 2022 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, amesema kuwa ugawaji wa pembejeo utazingatia eneo mkulima anapolimia, ukubwa wa shamba, idadi ya mikorosho pamoja na uzalishaji wa mkulima husika.
Aidha, pembejeo zitatolewa kwa wakulima kupitia kamati za pembejeo zilizoundwa kuanza ngazi ya taifa mpaka kijiji. Wakulima wote watatambulika wao na mahitaji yao kupitia mikutano ya kijiji ambayo itatoa maamuzi ya usambazaji wa pembejeo kwa wakulima wa kijiji husika.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa kwenye kikao hicho, mwenyekiti wa kikao Mhe. Hashim Komba, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea amewataka voingozi na watendaji kuhakikisha kamati zote zilizoelekezwa na muongozo zinaundwa kwa ngazi zote. Pia amezitaka kamati za vijiji zilizoundwa zihakikishe pembejeo hizo zinatolewa kwa walengwa kwa kutumia kanuni itakayomnufaisha kila mkulima.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msimu wa korosho wa mwaka 2022/2023 imelenga kusambaza viwatilifu kwa wakulima bure ambapo jumla ya tani 25,000 za sulpher, viwatilifu vya maji jumla ya lita milioni 1.5 watapatiwa wakulima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.