Mkoa wa Lindi umepokea fedha za miradi za maendeleo ya elimu na afya kutoka Serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan. Jumla ya Tsh. 12,946,259,969.24/= zimepokelewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya sekta ya Elimu na Afya Mkoani Lindi. Kati ya fedha hizo jumla ya Tsh. 8,100,000,000 zitatumika kwa ujenzi wa miundombinu ya elimu na Tsh. 4,846,259,969.24/= kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya afya.
Fedha hizo zimetolewa na serikali ikiwa ni mgawo wa nchi nzima kutoka kwenye jumla ya shilingi trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kufufua uchumi kwa sekta zilizopata athari za kiuchumi kutokana na madhara ya UVIKO-19 Tanzania.
Akizungumza na kamati za mkoa na wilaya zilizoundwa kutekeleza miradi hiyo katika kikao kazi kilichofanyika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa jumatano ya tarehe 27 Oktoba 2021, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amesema fedha za miradi ya elimu ndiyo ambazo ziko tayari kwa utekelezaji.
Aidha, Mhe. Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa fedha hizi kwa upande wa elimu zitatatua changamoto zote za uchache wa madarasa kwani bajeti iliyopangwa ni kujenga darasa pamoja na madawati yake. Katika kufikia malengo kwa pamoja amesisitiza jamii ishiriki katika kuzalisha mahitaji ya miradi hiyo ikiwemo tofali huku akizionywa halmashauri kuhakikisha fedha hizo zinatimiza malengo yaliyokusudiwa.
“Watu wetu tutanunua mchanga, tutanunua kokoto na hivi vitu vingine ambavyo vinapatikana na wale ambao wanatengeneza tofali nzuri tutanunua.” Amesema.
Fedha za UVIKO-19 kama ambavyo zinatambulika zimepelekwa katika halmashauri zote za Mkoa wa Lindi ili kuondoa adha ya wananchi kupitia sekta ya elimu na afya. Mpango wa utekelezaji wa miradi hiyo umepangwa kukamilika kufikia mwezi Desemba 2021.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.