Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kupambana na magonjwa ya kuambukiza na yasioambukizwa mahali pa kazi. Hayo yamebainika jana katika kikao cha kamati ya kitaifa na Mkoa ya kudhibiti VVU, UKIMWI na magonjwa sugu yasioambukizwa mahali pa kazi katika utumishi wa umma kilichofanyika Mkoani Lindi, ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Akizungumza wakati akifungua kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ndg. Xavier M. Daudi amewakumbusha wajumbe wa kamati hizo za kitaifa na mkoa kuzingatia utekelezaji wa Sheria ya UKIMWI ya mwaka 2008 pamoja na Mkakati wa Nne wa kudhibiti UKIMWI 2018-2023. Ameongeza kuwa Tanzania imelenga kuhakikisha inafikia lengo la Kimataifa la 95-95-95 ifikapo 2025 yaani ikimaanisha 95% ya wanaoishi na VVU wanatambua hali zao, 95% ya WAVIU wawe wameanza dawa ya kupunguza makali ya VVU na 95% ya walioanza dawa wapunguze kiwango cha virusi mwilini.
Katika kufikia malengo hayo Ndg. Xavier M. Daudi amezielekeza wizara na mikoa kuhakikisha zinatenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Afua za VVU, UKIMWI , kuwashauri Waajiri kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi na kupima afya za watumishi mara kwa mara.
“Suala la mazoezi ni kitu ambacho halihitaji raslimali fedha, hivyo tujenge utamaduni wa kushirikiana na kuhamasishana kufanya mazoezi ya mara kwa mara. Utaratibu huu utapunguza changamoto nyingi za kiafya kwani mazoezi ni tiba.” Amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Anuai za Jamii kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Mwanaamani Juma Mtoo akizungumza na waandishi wa habari amesema kuwa Lengo la kuja Mkoani Lindi ni pamoja na kuona Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri zake namna gani zinasimamia na kutekeleza Afua mahali pa kazi ili serikali iweze kufikia malengo yake kwa kuwa na wafanyakazi wenye afya bora. Amesema kuwa kupitia Sera ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2008, unaandaliwa mwongozo wa namna ya kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa sugu yasioambukizwa mahali pa kazi ambao pia utatumika kudhibiti matatizo ya msongo wa mawazo na matatizo ya akili.
Akisoma taarifa ya Mkoa wa Lindi na Halmashauri zake Katika kupambana na magonjwa VVU, UKIMWI na magonjwa yasioambukizwa Dkt. Bora Haule amesema kuwa jitihada mbalimbali zinafanyika ikiwemo utoaji wa elimu, kuhamasisha wafanyakazi kupima ili kufahamu afya zao, kusambaza kinga kwa wafanyakazi, kutoa chakula lishe, kutoa fedha kila mwezi kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa VVU.
Ikumbukwe kuwa vyanzo vikubwa vya magonjwa yanayoambukizwa na yasioambukizwa yanasababishwa kwa kiasi kikubwa na tabia zisizofaa ikiwemo ulaji usiozingatia utaratibu wa lishe bora, tabia za kutofanya mazoezi, ngono isio salama nk. Hii imesababisha kupungua kwa nguvu kazi na familiana taifa kwa ujumla hivyo kushusha uzalishaji na uchumi kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.