Serikali yafafanua uwepo wa kitengo cha uvunaji mamba na viboko.
Wizara ya Maliasili na Utalii nchini imethibitisha uwepo wa kitengo maalumu kinachojihusisha na udhibiti wa wanyamapori ambapo moja ya kazi yake ni uvuaji wa mamba na viboko.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu katika maonyesho ya nanenane yaliyofanyika kikanda katika viwanja vya Ngongo – Manispaa ya Lindi, alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya uwepo wa malalamiko ya uvamizi wa viboko katika maeneo ya Wananchi.
“Kitengo kipo na wanyama hao huvuliwa baada ya kukamilisha utafiti, hivyo baada ya malalamiko mengi kutoka mto Ruvuma na Rukwa tumeiagiza TAWA kufanya utafiti na kutuambia ni mamba na viboko kiasi gani tunaweza kuvuna”, alisema Mhe. Kanyasu.
Baada ya majibu ya tafiti kutoka taratibu za kutangaza tenda kwa ajili ya kuvuna na kuuza zitafuata kwani mamba na viboko ni chakula kama samaki.
Aidha, naibu waziri Kanyasu ameeleza mpango wa serikali wa kufungua mabucha yatakayouza nyama za wanyamapori katika maeneo mbalimbali nchini. Wizara imeanzisha utaratibu wa uwindaji wa ndani {resident hunting} ambapo nyama zitakazo kuwa zikipatikana zitakuwa zikiuzwa kwenye mabusha hayo.
Hii itasaidia wananchi kupata nyama za pori kwa urahisi pale wanapokuwa na uhitaji. Hivyo wawindaji watatakiwa kufuata taratibu za kuomba vibali kwa ajili ya kuwinda ambavyo vitaainisha aina ya wanyama ambao watakwenda kuwawinda.
Pia naibu waziri ameongeza kuwa wizara yake imeshaandaa kanuni na utaratibu utakaosimamia biashara hiyo ya nyama za wanyamapori na kuongeza kuwa mabucha hayo yanatarajiwa kufunguliwa mwaka huu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.