Watoa Huduma ngazi ya Jamii wametakiwa kuendelea kufanya kazi nzuri ya kuelimisha jamii kuhusu masuala mazima ya afya ili kuzidi kutoa chachu kwa wanajamii kuhudhuria katika vituo vya afya na hospitali wanapougua au kupata dalili za hatari pamoja na kupata elimu mtambuka.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Mkoa wa Lindi yenge lengo la kukagua hali ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wanajamii pamoja na utekelezaji wa miradi ya afya katika wilaya hiyo ambapo katika ziara hiyo Dkt. Magembe alitembelea katika Kituo cha Afya cha Liwale Mji na kujionea mchango mkubwa unaofanywa na Watoa Huduma za Afya ngazi za Jamii katika kutoa elimu inayowahamisha wananchi hususani akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki, kuhakikisha wanajifungua katika vituo vya afya na kutoa elimu ya unyonyeshaji pamoja na dalili za hatari zinazoweza kumpata mtoto na mama baada ya kujifungua.
Aidha, Dkt. Magembe ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya inatambua mchango wa watoa huduma kwa jamii kama kiunganishi baina ya wananchi na huduma za afya hivyo kuja na mpango maalumu wa kuwapatia elimu na ujuzi watoa huduma ngazi ya jamii ili kuweza kuwarasimisha.
"Serikali ya awamu ya sita imeandaa programu maalumu inayoitwa A Coordinated Intergrated Program of Community Health Workers ambayo inaenda kuwarasimisha watoa huduma ngazi ya jamii kwa kutangaza nafasi za kazi za wahudumu kutoka katika jamii husika wanazoishi kisha serikali itawapa mafunzo ya miezi sita wahudumu hao ili waweze kupata maarifa na ujuzi zaidi katika maeneo mbalimbali ikiwemo masuala ya Kifua Kikuu, VVU/UKIMWI, Malaria na Lishe, Water and Sanitation, Malezi na Makuzi ya Mtoto, miezi mitatu watakua darasani na miezi mitatu mingine watakua field ili kuhakikisha wanakua na ujuzi unaotakiwa" Ameeleza.
Bi Somoe Ngaokola ni mtoa huduma kwa jamii chini ya Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka MSF linalotoa huduma za afya ya Mama na Mtoto katika kituo cha afya cha Liwale Mji anaeleza namna ambavyo anatoa elimu juu ya huduma za afya hususani kwa wamama wajawazito, malezi ya watoto na elimu mtambuka.
"Kupitia MSF tumewezeshwa kwa kupata mafunzo ambayo yametuwezesha kuwahudumia wanajamii wenzetu katika masuala mbalimbali hususani kuelimisha na kuwashawishi wanawake kuhudhuria kliniki wanaposhika ujauzito lakini pia elimu ya unyonyeshaji wa watoto haswa umuhimu wa kunyonyesha mtoto miezi sita bila ya kumpatia kitu kingine chochote kama vile maji, dalili za hatari kwa mtoto kama degedege na dalili za hatari kwa mama baada ya kujifungua kama vile kuvimba miguu na mwili kubadilika rangi wasikimbilie kwa waganga wa kienyeji waje hospitali kupata huduma kwa maana hizo ni dalili za kifafa cha mimba hawajarogwa pamoja na elimu nyinginezo mtambuka ikiwemo usafi"
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.