Wananchi na wanafunzi wa kitongoji cha Namdeda,Kijiji cha Mtua longa, kata ya Longa, Halmashauri ya Mtama wamenufaika na mradi wa maji safi na salama baada ya shirika la Heart to Heart kwa kushirikiana na shirika la Smart HB kuwajengea kisima cha maji kilichogharimu kiasi cha shilingi Milion 20.
Katika hafla ya kukabidhi mradi huo unaotekelezwa katika katika Shule ya Msingi Namdeda na kuwekewa jiwe la msingi na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Victoria Mwanziva, wananchi wameishukuru Halmashauri ya Mtama kwa kushirikiana na shirika hilo kwa kuwajengea kisima hicho ambacho kinaenda kuwa mkombozi wa kutatua changamoto ya maji iliyokuwa inawakabili hususan msimu wa kiangazi ambapo iliwalazimu kutembea umbali wa takribani Km 10 hali iliyosababisha kuzorota kwa shughuli nyingine za kimaendeleo ikiwemo elimu huku shule ikiendesha shughuli zao kwa hali ngumu ikiwemo ujenzi wa madarasa.
Akieleza kuhusu mradi huo Meneja wa mradi kutoka Shirika la Heart to Heart Ndugu. Deodatus Banzi ameeleza kuwa shirika limejikita zaidi katika kutatua changamoto za sekta ya afya na usafi wa mazingira ambapo katika kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha ubora wa huduma za afya, usafi wa mazingira na huduma za kijamii, shirika limefanikiwa kujenga visima 34 katika maeneo mbalimbali ya Mtama huku ikiazimia kujenga visima vingine 14 kwa miaka mitatu ijayo na kufanikiwa kuzifikia kata 20 ambazo wamezihamasisha na kuwachangia vifaa vitakavyowawezesha kujenga na kutumia vyoo bora
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe Victoria Mwanziva amewahimiza wananchi kutunza mradi huo ili huduma hiyo ya maji safi na salama uweze kuwanufaisha kwa muda mrefu. Aidha, Mhe. Mwanziva amewahimiza wananchi wa kitongoji cha Namdeda kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji wa daftafi la wapigakura wa serikali za mitaa linalotarajia kuanza ifikapo Oktoba 11-20 2024 na kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa ifikapo Novemba 27, 2024.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.