Kutokana na kuwepo kwa teknolojia mbalimbali za kuongeza thamani katika mazao,serikali imeendelea kuhamasisha wadau na wakulima nchini kuwekeza katika zao la korosho na kuliongezea thamani ili kupata faida zaidi.
Watafiti wa Kilimo kutoka taasisi ya utafiti Tari Naliendele wanaeleza uwekezaji unaohitajika ni katika viwanda vya ubanguaji na uongezaji wa thamani wa korosho ghafi huku matunda yake (mabibo)ambayo mkulima kwa sasa huyaacha shambani kwa kiasi kikubwa na kiasi kidogo ukitumia kutengeneza pombe za asili kama Nipa na ulaka yanatajwa kuwa na faida kubwa kiuchumi.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack ambaye ni mgeni rasmi katika siku ya Korosho iliyofanyika Agosti 5,2023 katika Jengo la Bodi ya korosho, Nanenane Kanda ya Kusini,Ngongo amehamasisha wananchi kula bidhaa za korosho akisema ulaji wa bidhaa zinazotokana na korosho na bibo litasaidia kuongeza ajira kwa vijana,kutunza soko la ndani ,kuimarisha afya,kutanua ongezeko la mahitaji nchini na hivyo kuongeza ushindani kati ya mahitaji ya korosho ya ndani na nje jambo litakalosaidia Mkulima kunufaika na bei nzuri.
Bakari Kidunda, Kaimu Mkurugenzi wa Tari Naliendele Mtwara, amesema korosho inathamani kuanzia kwenye korosho karanga (ndani),ganda lake la nje hadi tunda lake ambalo likiongezwa thamani kwa kilo moja ya mabibo inauwezo wa kutengeneza chupa moja ya mvinyo na kuuzwa.
Awali,Mwenyekiti wa bodi ya korosho Aloyce Damian Mwanjire ametaja miongoni mwa bidhaa zinazoweza kuzalishwa na korosho kuwa ni pamoja na Maziwa ambayo amedai kuwa yana virutubisho vingi ambavyo vinasaidia kudumisha Ndoa na mahusiano.
Siku ya korosho hufanyika kila inapofika Agosti 5 kila mwaka ikiwa na lengo la kuhamasisha uwekezaji na ulaji wa bidhaa zinazotokana na zao la korosho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.