Bodi ya Korosho Tanzania kwa kushirikiana na taasisi ya Utafiti Naliendele (TARI), jana tarehe Agosti 05, imeadhimisha siku ya Korosho pamoja na kuzindua kampeni ya Ulaji na Utumiaji wa bidhaa zitokanazo na zao hilo ikiwemo maziwa, mvinyo na sharubati itokanayo na Korosho kama njia ya kutoa msukumo uzalishwaji wa zao hilo kwa wingi na kwa kuzingatia ubora na viwango vya kimataifa.
Awali Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, amesema “Takwimu zinonyesha ubanguaji wa korosho hadi sasa ni sawa na asilimia mbili tu hivyo inakua ngumu kufikia lengo la asilimia sitini ya ubanguaji ifikapo 2024/2025 ikiwa sisi wenyewe hatutumii kile tunachozalisha kwa wingi hivyo maadhimisho ya siku ya korosho yanafanyika ili kuhamasisha matumizi ya korosho kuanzia kwa soko la ndani ya nchi na bidhaa zake nyingine pia kuvutia zaidi wawekezaji”
Aidha, Kaimu Meneja Idara ya Uchumi Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Bwana Aristedes Mrema, amesema kuwa Benki Kuu inakitazama kilimo cha Korosho kama zao muhimu sana kwa ustawi wa nchi na ustawi wa uchumi kwa mikoa ya kusini kwani licha ya kuongeza kipato kwa mwananchi mmoja mmoja katika ukanda huu pia ni moja ya zao la kimkakati linaloiingizia nchi fedha za kigeni.
“Kiasi cha Korosho kinachobanguliwa hapa nchini ni takribani ya asilimia kumi tu ya korosho zote zinazopatikana hapa nchini kwa mwaka, jambo hili linaipotezea nchi fedha nyingi sana hivyo juhudi kama hizi za kuipa thamani korosho hapahapa nchini ni jambo lenye manufaa kwa nchi kiuchumi na kijamii pia.” Ameongeza Mrema.
Kanali Ahmed Abbas, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambaye ndiye Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ya Siku ya Korosho yaliyofanyika katika viwanja vya maonyesho ya Nanenane kwa kanda ya Kusini, Ngongo, ameipongeza Bodi ya Korosho na Taasisi ya Utafiti Naliendele (TARI) kwa tafiti mbalimbali wanazozifanya zenye tija kwenye mazao mbalimbali ya kilimo ikiwemo zao la Korosho.
“Kiupekee niwapongeze sana Bodi ya Korosho na TARI Naliendele kwa kuandaa na kuazimisha siku hii ya Korosho na kupitia tafiti hizi zilizofanywa zitokanazo na korosho hapa tumepata mvinyo, maziwa ambayo yanatokana na Korosho,na utaratibu huu utachochea sana kukua kwa sekta ya ujasiriamali na katika namna ya pekee sana utaongeza na kuchochea mnyororo wa thamani wa zao la Korosho” amesema Kanali Abbas.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.