Katika kuadhimisha siku ya macho duniani, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine kwa kushirikiana na Shirika la Heart to Heart Foundation, Korean Church na CBM wamewafikia wananchi wapatao 10,378 mkoani Lindi kwa kuwapa huduma ya elimu ya afya ya macho huku kati yao 9690 wamefanyiwa vipimo na kupatiwa matibabu kupitia kambi mbalimbali zilizoendeshwa katika wilaya zote za Mkoa wa Lindi.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Sokoine Dkt. Sharifu Hamza ameeleza kuwa zoezi hilo lililoendeshwa kwa siku saba kuanzia oktoba 4 hadi 7 wataalamu walipita katika shule mbalimbali za halmashauri zote sita kutoa elimu pamoja na kutoa matibabu kwa wananchi na wanafunzi walioonekana na changamoto ya afya ya macho na kuongeza kuwa imekua ni faraja kwa wananchi kusogezewa huduma bora za macho hivyo zoezi hilo limekuwa na mafanikio makubwa.
Bwana. Edward Aloyce Afisa mradi kutoka shirika la Heart to Heart Foundation amesema shirika lao limekuwa likifanya mradi wa macho katika Mkoa wa Lindi na kuongeza kuwa katika kambi ya mwaka huu wamelenga kupata watoto 20 wenye changamoto ya mtoto wa jicho ambao watanufaika kwa kupata huduma ya operesheni bure.
"Tumesukumwa kwa sababu watoto ndio wanapata changamoto kubwa katika tatizo la macho na tumefanya kwa ushirikiano pamoja na hospitali hii ya Lindi Sokoine lakini pia tutafanya na hospitali ya taifa ya muhimbili kwa kuleta madaktari bingwa baada ya watoto hao kuweza kuhainishwa kutokana na changamoto zao za magonjwa ya macho"
Hata hivyo, Aloyce ametoa wito kwa wananchi, wazazi na watoto kujenga tabia kufanya uchunguzi wa changamoto za macho katika hospitali ili kujikinga na maradhi mbalimbali ya macho yanayoweza kuleta athari kubwa ikiwemo upofu.
Dokta. Mwacha Machaja, Mtaalamu wa huduma za macho Mkoa na Hospital ya Rufaa ya Lindi Sokoine amesema zipo sababu mbalimbali zinazopelekea matatizo ya macho ambapo miongoni kwa sababu hizo ni umri, ajali, lishe duni , maambukizi na sababu za kuzaliwa.
"Wakazi wengi wa Lindi wanaopata changamoto ya macho inatokana na kutokula vyakula vinavyolinda macho hususani kuimarisha ukuta wa jicho na mishipa ya fahamu ikiemo mboga za majani ambazo hazijapikwa sana kiasi cha kupoteza rangi yake pamoja na karoti iliyopikwa"amefafanua.
Siku ya Macho Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo Oktoba 10 ambapo kwa mwaka huu maadhimisho hayo yamepambwa na kauli mbiu isemayo 'Penda Macho Yako, Muhamasishe Mtoto Kupenda Macho Yake' imelebga zaidi kuhamasisha watoto na wanafunzi kupenda na kujari afya ya macho kwa kuwapa elimu mbalimbali juu ya afya ya macho na namnq ya kujikinga dhidi ya maradhi ya macho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.