WANANCHI WAZAWA WATAKIWA KUJENGA TABIA YA KUTEMBELEA HIFADHI ZA WANYAMAPORI NA MAENEO YA KIHISTORIA.
Kuelekea katika Maadhimisho ya Maonyesho ya 31 ya Nanenane, leo Agosti 4, 2024 Mikoa ya Lindi na Mtwara imeadhimisha Siku ya Mazingira na Maliasili ambapo Mhe. Michael Mtenjele, Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba na mgeni rasmi katika siku hiyo amewaasa wananchi kutumia fursa ya uanzishwaji wa mabucha ya nyamapori kujiongezea kipato na kuwinda wanyamapori kwa kufuata sheria na utaratibu.
"Wenzetu wameonyesha njia inayotuonyesha kwamba tunaweza kupata mazao ya maliasili na nyamapori kwa kufuata utaratibu unaokubalika kisheria badala ya kuingia kiujangili na kwenda kuwinda bila ya utaratibu. Hivyo wameturahisishia kwakua sasa unaweza kufanya biashara hii kwa kukata kibali cha kuwinda na kuuza nyamapori kwa uwazi kabisa bila ya kujificha" Amesema.
Aidha, Mhe. Mtenjele ameeleza kuwa kuna fursa nyingi zinazopatikana katika shughuli za uhifadhi ikiwemo bustani za wanyamapori hivyo wananchi wazawa wajenge tabia ya kutembelea vivutio mbalimbali ikiwemo maeneo ya uhifadhi, maeneo ya kihistoria na mbuga za wanyama.
Vilevile, wananchi wametakiwa kujenga tabia ya kutumia mazao mbalimbali ya misitu yaliyoongezewa thamani ikiwemo fenicha kama vitanda, milango na viti ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wazalishaji ambazo huchangia kuongeza pato kwa taifa.
Mwisho, Mhe. Mtenjele amewataka wananchi kuhakikisha wanashiriki katika shughuli za uhifadhi wa mazingira kwa kuacha kukata miti kiholela, kupunguza matumizi ya mkaa na kuni na uwindaji haramu.
TUMERITHISHWA, TUWARITHISHE.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.