Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi aliyekuwa mgeni rasmi kwenye kikao cha mafunzo ya matumizi ya takwimu za Sensa iliyofanyika 2022 amesema kuwa kwa sasa maamuzi yote yanayofanywa ni lazima yazingatie ushahidi wa kitakwimu kupitia matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Mhe. Ndemanga ameyasema hayo katika kikao cha mafunzo ya matumizi ya takwimu zilizopatikana kupitia sensa ya watu na makazi iliyofanyika agosti 2022 ambacho kilifanyika ijumaa ya tarehe 26 Mei 2023 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Mhe. Ndemanga amesema kuwa sasa wakati wa kufanya maamuzi kwa mitazamo, maoni au nguvu ya watu umekwisha na badala yake maamuzi yote yafanyike kwa kuzingatia uwiano wa takwimu Kati ya eneo moja na lingine.
Amesisitiza kuwa hakuna haja ya kutumia nguvu kwenye maamuzi ya upelekaji wa huduma za jamii Kati ya kijiji kimoja na kingine kwa kuwa uwingi wa watu ndio utakaoamua ni wapi huduma zielekezwe.
Mhe. Ndemanga ameongeza kuwa takwimu za Sensa zimesaidia katika maandalizi ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2023/24 ambapo vipaumbele vimezingatia matokeo ya Sensa ya mwaka 2022.
Mhe. Ndemanga ameendelea kusema kuwa Sensa ya mwaka 2022 imeonesha ongezeko kubwa la watu kwa Mkoa wa Lindi ambapo takribani watu zaidi ya laki 3 kutoka wameongezeka ukilinganisha takwimu za Sensa iliyofanyika mwaka 2012 ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.2.
Kwa upande wake Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Spika wa Bunge Mstaafu Mhe. Anna Makinda amewaasa Vijana kuachana na matumizi mabaya ya simu na badala yake watumie takwimu za Sensa hasa za anwani za makazi kufanya biashara kidigitali.
Mhe. Makinda amewataka Vijana kubadilika ikiwemo kutumia takwimu za Sensa kupanga mipango ya maendeleo na kuachana na tabia ya kukaa vijiweni kupiga soga.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Bi. Zuwena Omary amewasisitiza wananchi kuzitumia takwimu za Sensa kutoka kwenye chanzo sahihi na kuachana na takwimu ambazo hazijathibitishwa na mamlaka husika.
Wadau mbalimbali wa Mkoa wa Lindi wamepatiwa mafunzo ya namna ya kutumia takwimu za Sensa ya mwaka 2023 kupitia muongozo uliokwisha zinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. Aidha, mafunzo hayo yamefanyika Leo ijumaa tarehe 26 Mei 2023 katika ukumbi mkubwa wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.