TANESCO Kanda ya Kusini yaagizwa kuuangaliaa upya mgao wa umeme kwa Mkoa wa Lindi.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi amemuagiza Meneja wa TANESCO Kanda ya Kusini kuuangalia upya mgao wa umeme kwa Mkoa wa Lindi kwani umeme umekuwa ukikatika kila wakati.
Mhe. Zambi alikwenda Mkoani Mtwara kwa lengo la kukutana na uongozi wa TANESCO Kanda na Kituo cha Uzalishaji Umeme, pia kukutana na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kusini, na Uongozi wa Bandari ya Mtwara.
Alipokutana na uongozi wa TANESCO, Mhe. Zambi aliwaeleza kuhusu tatizo la kukatika kwa umeme kwa mkoa wa Lindi ambapo aliwataka wampatie maelezo ya nini kinasababisha umeme kukatika mara kwa mara katika Mkoa wa Lindi ambapo ndani ya muda mfupi umeme unaweza kukatika hata mara kumi.
Meneja wa Kituo cha Uzalishaji Umeme, Mhandisi Chinumba alieleza kuwa uzalishaji wa umeme kwa sasa umeshuka kutokana na mitambo mitatu kati ya tisa kuzimwa kutokana na uzalishaji wake kushuka sana ambayo inahitaji kufanyiwa matengenezo muhimu. Hivyo mitambo inayofanya kazi kwa sasa ni sita japo kati ya hiyo mitambo miwili haifanyi kazi kwa asilimia 100.
Juhudi za kuhakikisha vifaa/vipuri vinapatikana kwa haraka zinaendelea ambapo mpaka sasa vipuri vya kuwezesha matengenezo ya mtambo mmoja tayari vimefika na matengenezo yaaendelea. Mitambo mingine mitatu matengenezo yake yataanza mara tu bada ya kupokea vipuri husika.
Vilevile TANESCO wameshaagiza mitambo mingine miwili ambayo itafua umeme wa jumla ya 4MW ambayo inatarajiwa kuanza kazi February 2018. Hivyo ikiwa mitambo yote itakuwa inafanya kazi uzalishaji wa umeme utakuwa ni 22MW ambapo kwa sasa uzalishaji ni 18MW.
Mhe. Zambi alitembelea kituo cha uzalishaji na kuona mitambo yote huku mafundi wakiwa wanaendee kufanya matengenezo ya mtambo mmoja. Kikubwa alichowaagiza uongozi wa tanesco kanda ni kuangalia upya tatizo la kukatika umeme mara kwa mara katika mkoa wa Lindi na kwamba kama kuna mgao basi uwe sawa kwa mikoa yote.
Pia Mhe. Zambi aliongea na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kusini ambapo alizungumza nae kuhusu mgogoro wa mipaka kati ya Kikosi cha 41KJ na wananchi na Kikosi cha 843KJ na wananchi, vilevile alizungumzia mgogoro wa ardhi uliopo kilwa eneo lililotaka kulimwa Mibono.
Baada ya hapo Mhe. Zambi alitembelea bandari ya mtwara ili kuona hali ya bandari ilivyo kwa sasa hasa ukichukulia huu ndio msimu wa korosho ambapo wafanyabiashara wengine hutumia bandari hiyo kusafirishia korosho. Hali aliyoikuta ameridhishwa nayo kwani amekuta makasha yapo ya kutosha, nafasi ipo ya kutosha na meli zinaendelea kupakia mzigo.
Hivyo amewatoa hofu wafanyabiashara ambao walikuwa na wasiwasi wa kutumia bandari ya mtwara kwani kwa sasa maboresho makubwa yamefanyika. Aidha, ametembelea kuona maandalizi yanayofanyika kwa ajili ya kuanza kuongeza ukubwa wa gati ili kuongeza idadi ya meli zitakazokuwa zikipakia au kushusha mzigo kwa wakati mmoja kwani kwa sasa ni meli mbilli tu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.