Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack ameiagiza wakala wa barabara za vijijini na mijini (TARURA) wilaya ya Kilwa kumsimamia mkandarasi wa kampuni ya MS ERIT INVESTMENT GROUP LIMITED anayetekeleza mradi wa barabara ya Hoteli tatu - Pande na kuhakikisha anamalizia kasoro ndogondogo zilizopo katika mradi huo katika kipindi chake cha matazamio ili iweze kutumika katika kipindi chote cha mwaka.
Mkuu wa Mkoa ametoa agizo hilo alipotembelea na kukagua barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 14, na kubaini baadhi ya kasoro ambapo amesema kama zisiposimamiwa kikamilifu na kufanyiwa marekebisho yatakwamisha lengo la serikali la kuwaondolea wananchi wa Hoteli tatu hadi Pande changamoto ya usafiri hasa kwa wakati wa masika
“Hii barabara inatakiwa iwe inapitika katika kipindi chote cha mwaka,na serikali imeshatoa fedha kwa ajiri ya kutengeneza miundombinu ya barabara hii sasa niwatake TARURA kumsimamia mkandarasi aweke kifusi kinachofaa hapa na katika kipindi hiki cha mvua arudi site ili aangalie sehemu korofi za yeye kuweka kuweka mitaro inayotakiwa ili maji yasilale barabarani na kuweka madimbwi. Wananchi wanalalamika na mimi nisingependa kuendelea kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakato serikali ilishatoa fedha na wananchi wakizidi kulalamika maana yake kuna mapungufu sasa rekebisheni hayo mapungufu ili hii barabara ipitike” amesema Mkuu wa Mkoa.
Kwa upande wa Kaimu meneja wa TARURA wilaya ya Kilwa, Mhandisi David Geofrey amesema kuwa mradi huo wa barabara unajumuisha Kilometa 10 kutoka Mkazambo hadi Pande na Kilometa 4 kutoka Mkazambo hadi Lihimilo ulianza utekelezaji wake mwezi Februari 7, 2022 na kukamilika August 1, 2022 ukiwa umegharimu kiasi cha Shilingi za Tanzania Milioni 500 zilizotokana na tozo za mafuta.
“Baada ya mradi kukamilika, mkandarasi kwa sasa yupo katika kipindi cha matazamio kabla ya mradi huu kuukabidhi rasmi, na kulingana na kasoro hizi zilizojitokeza mkandarasi atatakiwa kurudi eneo la mradi na kuzifanyia marekebisho ambapo itajumuisha na kuchimba mifereji. Sisi TARURA tayari tumeshamuandikia barua ya kumtaka arudi site ili kufanya marekebisho hayo” Mhandisi David Geofrey.
Naye diwani wa kata ya Pande, Mhe. Selemani Waziri ameiomba TARURA kusimamia marekebisho hayo kwa wakati muafaka sambamba na kumalizia kutengeneza kipande kilichobakia chenye umbali wa Mita takribani 600 ili wananchi wa kata yake waondokane na adha ya usafiri wa watu pamoja na mazao hasa katika kipindi cha masika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.