Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya barabara katika mkoa wa Lindi wametakiwa kumaliza kazi kwa wakati na kwa matakwa ya ubora inayowekwa katika mikataba yao ya kazi wanayokabidhiwa.
Hayo yameelezwa katika kikao cha robo ya kwanza cha Bodi ya Barabara (Road Board) mkoa kwa mwaka 2022/2023 kilichofanyika tarehe 10 Januari, 2023 katika ukumbi wa mkutano, ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Lindi ambapo wadau na wajumbe wa walioshiriki kikao hicho wameitaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kutafuta wakandarasi wenye sifa na weledi wa kufanya kazi hizo.
Mhe. Hashim Komba, mkuu wa wilaya ya Nachingwea amesema “Naomba sana mnapotafuta wakandarasi tuwatafute wakandarasi wenye sifa na uwezo, muda mwingi tunajikuta tunautumia kwenye kuwatafuta na kuwafatilia wakandarasi kuliko kutafakari shughuli za maendeleo katika maeneo yetu, unakuta mkandarasi amekabidhiwa site haiingii kazini kwa wakati na hadi mradi utekelezeke ni kazi kubwa kwelikweli, vilevile tuangalie na vigezo vya kuwapa kazi wakandarasi hawa tusiwape kazi nyingi wakati uwezo wao ni mdogo tunajikuta tunakwamisha kazi hizi zaujenzi wa barabara zetu”
Mhandisi Filbert Mpalasinge, Meneja wa TARURA Mkoa wa Lindi amesema kuwa wamejipanga vya kutosha katika kuangalia uwezo wa wakandarasi wanaoingia nao mikataba ya kazi ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia ubora na kuikamilisha kwa wakati unaopangwa.
“Sisi kama TARURA tumejipanga vizuri kabisa kwa kuanzia na mchakato wa manunuzi ili kuhakikisha tunapata wakandarasi wanaofaa laiki pia kuwasimamia ipasavyo wale ambao wanakuwa wameshapata kazi kwa maana ya tunaoingia nao mkataba wa kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara”
“Katika kipindi hiki cha masika tumejipanga vizuri kabisa kutembelea na kukagua barabara zote korofi na kwenye madaraja ili sehemu ambazo zitabainika kuwa korofi tuzipatie ufumbuzi mapema na kuwawezesha wananchi kuzitumia barabara hizo bila usumbufu wala changamoto yoyote katika majira haya ya mvua” ameongeza Mhandisi Mpalasinge.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.