Tathmini ya mahitaji ya magunia ya kuwekea korosho kufanyika Lindi.
Viongozi katika Wilaya za Mkoa wa Lindi wameagizwa kufanya tathmini halisi ya mahitaji ya magunia ya korosho itakayozingatia makisio ya makusanyo ya korosho katika vya Msingi (AMCOS).
Maagizo hayo yameolewa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi alipofanya ziara katika Wilaya za Liwale, Rungwa na Nachingwea ambapo alikuta korosho nyingi zikiwa kwenye vyama vya msingi huku nyingine zikiwa zimemwagwa chini katika maghala kutokana na kukosekana kwa magunia ili zipelekwe katika maghala makuu.
Mhe. Zambi aliamua kufanya ziara ya kutembelea vyama vya msingi na maghala makuu baada ya kupata malalamiko ya upungufu wa magunia. Katika ziara yake alibaini kuwa ni kweli upungufu wa magunia upo lakini pia utaratibu wa ugawaji wa magunia yaliyotolewa mwanzo kwa baadhi ya vyama haukuwa mzuri.
Katika Wilaya ya Liwale wapo baadhi ya wakulima walichukua magunia mengi kuliko uwezo wao wa kuzalisha ambapo baada ya timu ya ufuatiliaji kufanya kazi ilibaini magunia 3,401 yapo kwa wakulima bila kuwa na kurosho.
“Nawaagiza Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Lindi kuhakikisha wanafanya tathmini za mahitaji halisi ya magunia na kuiwasilisha kwani nimeshaongea na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho ambaye anahitaji kupata mahitaji halisi ili aweze kutafuta magunia na kuyaleta”, alisema Mhe. Zambi. Vilevile aliagiza tathmini itakayofanyika iangalie matumizi ya magunia yaliyotolewa awali.
Pia aliawagiza viongozi wote wa vyama vya ushirika kuanzia vyama vikuu na vya msingi na viongozi wa wilaya kuhakikisha wanasimami utaratibu wa matumizi ya magunia. Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho alimuahidi Mhe. Zambi kuwa atapeleka magunia 25,000 ndani ya siku mbili ili kusaidia kupunguza upungufu uliopo wakati tathmini inafanyika.
Vilevile Mhe. Zambi amemuagiza Kamanda wa Polisi Wilaya ya Liwale kuwakamata na kuwahoji viogozi wa chama cha msingi mshikamano ambao kwanza walikuwa wanahamisha mzani kwenda kwa wakulima kuwapimia korosho wakati utaratibu unawataka wasihamishe mzani kwani kwa kufanya hivyo husababisha mzani kucheza na kutopima sawasawa.
Pili ni taratibu walizotumia kugawa magunia kwani baada ya mkulima mmoja kutembelewa alikutwa akiwa na magunia 10 ambayo hayatumii kutokana na kuishiwa korosho. Lakini pia utaratibu unataka mkulima asipewe magunia mpaka apeleke korosho zake katika ghala la chama cha msingi ambapo korosho zitachambuliwa na kuwekwa katika magunia.
Aidha, Mhe. Zambi amemuagiza Kamanda wa Polisi Liwale kuwakamata na kuwahoji viongozi wote wa vyama vya msingi ambao waliacha korosho zao zinaharibika nje ya ghala kuu la Umoja bila kuzichambua kama utaratibu unavyotaka.
“OCD nakuagiza uwakamate viongozi wa vyama vya msingi ambao wameacha korosho za wakulima zinaharibika hapa nje badala ya kuja kuzichambua na kuziingiza ndani ya ghala”, alisema Mhe. Zambi.
Katika Ziara yake hii Mhe. Zambi aibaini baadhi ya changamoto zilizopo katika Maghala Makuu ambapo katika ghal la Umoja Wilayani Liwale aliwashauri waongeze milango mingine miwili kwani kwa sasa upo mmoja hivyo inakuwa ngumu kazi ya kupakia na kushusha kufanyika kwa wakati mmoja.
Na katika ghala la Lindi Farmers Wilayani Nachingwea aliwashauri kubadilisha utaratibu wa upakiaji na ushushaji unaotumika na sasa kuwa na siku moja ya kupakia na siku moja ya kushusha. Aidha, alimuagiza mtunza ghala kuhakikisha anachimba choo kipya ndani ya wiki mbili kwani vyoo vilivyopo havipo katika mazingira mazuri.
Pia alikuta tatizo la baadhi ya wanunuzi kutochukua korosho zalizonunua kwa wakati na kusababisha msongamano katika ghala ambapo alimuagiza Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji kuhakikisha tar. 15/12/2017 anawaita wanunuzi wanaohusika ikiwa ni pamoja na wanunuzi ambao hawajalipa fedha za wakulima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.