Tatizo la Umeme na Maji kumalizika Julai, 2017
Wakandarasi wanaojenga miradi ya maji na umeme katika Manispaa ya Lindi kwa pamoja wamemuhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi kuwa miradi hiyo itakamilika ndani ya Julai, 2017.
Wakandarasi waliyasema kwa nyakati tofauti wakati Mhe. Zambi alipotembelea miradi hii. Wakati akiwa katika mradi wa maji wa Ng’apa Mhe. Zambi aliridhishwa na kasi ya ujenzi inayoendelea na kumtaka Mkandarasi huyo kukamilisha kazi kwa wakati. Ujenzi wa mradi wa maji wa Ng’apa unagharimu shilingi bilioni 29 na unajengwa na kampuni ya Overseas Infrastructure Alliance ya nchini India.
Pia Mhe. Zambi alitembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme cha Maumbika ambapo mkandarasi alimueleza kuwa ujenzi wa njia kuu ya umeme kutoka Mtwara mpaka Maumbika umekamilika. Aidha, alieleza kuwa ujenzi wa miundombinu katika kituo unakwenda vizuri na wanauhakika kuwa ndani ya Julai, 2017 tatizo la umeme litakuwa limekwisha. Mradi huu unagharimu shilingi bilioni 16 na unajengwa na kampuni ya Electrical Transmission and Distribution Company (ETDCO).
“Tatizo la kukatika kwa umeme limekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wa Lindi, hivyo ni imani yangu kuwa mtaifanya kazi hii kwa umakini ili mradi utakapokamilika tatizo hili lisijirudi kabisa”, alisema Mhe. Zambi.
Vilevile Mhe. Zambi alitembelea mradi wa ujenzi wa maegesho ya kivuko cha Kitunda ambapo alikuta kazi ya ujenzi ikiwa inaendelea vizuri. Kampuni inayojenga mradi huu ni M/S Hematech Investment Ltd, Ira General Enterprises Co. Ltd JV na inajenga kwa gharama ya shilingi bilioni 1.9. Mradi huu unatakiwa kukamilika mwenzi Novemba, 2017 ambapo mkandarasi alimuhakikishia Mkuu wa Mko kuwa mradi utakamilika kwa wakati.
Baada ya kutembelea miradi yote hii, Mhe. Zambi aliwataka wanalindi kuwa na imani na serikali yao kwani inazifanyia kazi kero zao. Pia alisema kuwa serikali inaleta fedha nyingi Lindi kwa ajili ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushughulikia kero za wananchi ambapo alitoa mfano mdogo tu wa jumla ya fedha zinazotumika kutekeleza miradi hii mitatu.
Aidha, Mhe. Zambi aliwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika kujiletea maendeleo na katika kutafuta ufumbuzi wa kero mbalimbali zinazowakabili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.