Tutumie maghala makuu kudhibiti upotevu wa mazao - RC Zambi
Mkuu wa mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi amewataka viongozi na wadau wa ufuta kufikiria kutumia kutumia maghala makuu ili kudhibiti upotevu wa zao hilo.
Zambi ameyasema hayo katika kikao cha tathmini ya ununuzi wa zao la la ufuta ambapo taaarifa imeonyesha kuwepo na upotevi/wizi wa ufuta kwenye baadhi ya maghala ya vyama vya ushirika vya msingi na kusababisha wakulima kutolipwa fedha zao kwa wakati.
Katika taarifa iliyowasilishwa na mrajisi msaidizi wa mkoa, Ndg. Robert Nsunza imeonyesha kuwa upotevu huu umesababishwa na baadhi ya makarani na viongozi wa AMCOS kupoteza mizigo mfano vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) ya Nanjilinji imepoteza tani 81 za ufuta na viongozi wake kusingizia wameibiwa na chama kikuu, jambo ambalo sio la kweli kutokana na taarifa iliyotolewa na kamati ya uchunguzi iliyoundwa. Uzidishwaji wa mizigo kwa makampuni ambapo kampuni ya Hashim and SONs imezidisha tani 32 za ufuta kutoka wilaya ya Kilwa. Pia utoroshwaji wa mizigo bila kulipiwa ushuru.
Nsunza alisema kuwa tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuunda kamati za uchunguzi, kuwafikisha katika vyombo vya usalama viongozi waliohusika na upotevu huo, na kwa kampuni zilizozidisha mzigo na ambazo zimekiri kosa hilo wamelipia fedha za mizigo hiyo. Pia mikakati ya kuhakikisha wanunuzi wanalipia na ushuru wa halmashauri kulingana na kiasi cha mzigo waliozidisha imefanyika.
Nae Mkuu wa wilaya ya Nachingwea. Mhe. Rukia Muwango amelalamikia kitendo cha baadhi ya wazabuni kuchelewa kuchukua mizigo yao kwenye ghala za AMCOS na kusababisha hasara kwani maghala yaliyodhaifu hubomoka na mizigo inayoanguka husababisha ufuta kumwagika. Pia ameomba kurejeshwa kwa ushuru wa shilingi moja ambao ulikuwa unasaidia sana kwa shughuli za usimamizi na ufuatiliaji ambao ulisaidia kutokuwa na malalamiko ya upotevu/wizi katika msimu uliopita.
Aidha, Mkuu wa wilaya ya Lindi, Mhe. Shaibu Ndemanga amezitaka mamlaka husika kuchukua hatua za haraka wanapobaini tatizo kuliko kusubiri mpaka mwisho ndipo wavitake vyama kurejesha fedha. Wakati mkuu wa wilaya ya Kilwa, Mhe. Christopher Ngubiagai ametaka viongozi waliohusika/kusababisha upotevu huo kuchukuliwa hatua kali.
Meneja wa RUNALI Ndg. Hassan Mpako ameziomba mamlaka husika kuandaa sheria kali kuwabana viongozi wa Ushirika hasa makarani kwani wengi ndio husababisha upotevu huo. Pia ameomba elimu kuendelea kutolewa kwa makarani kwani wengi wao hawana elimu ya uhasibu na wenye taaluma hiyo hawataki kufanya kazi katika vyama vya ushirika kutokana na madhaifu yaliyopo.
Akihitimisha kikao hicho mkuu wa mkoa Zambi amewataka wadau kufikiria kuanza kutumia utaratibu wa maghala makuu licha ya utaratibu huu kutopendwa na baadhi ya wadau na wakulima. Njia hii itasaidia kudhibiti upotevu uliojitokeza msimu huu na pia kuwarahisishia wanunuzi kuchukua mzigo katika sehemu moja. Pia ameagiza kufanyika kwa ukaguzi katika vyama ambavyo vimehusika na upotevu ili kubaini hesabu kamili ya wakulima wangapi walistahili kulipwa kiasi gani cha fedha lakini kutokana na upotevu huo hawajalipwa. Lakini kwa watu ambao ufuta wao ulikamatwa na waliandika barua ya kukiri, ufuta huo uuzwe na pesa yake itumike kuwalipa wakulima.
Aidha, Mhe. Zambi ameagiza kufungwa kwa akaunti za makarani, makatibu na wajumbe wote wa AMCOS zenye upotevu ili kupisha uchunguzi, huku akiwataka maafisa ushirika kutoa majina ya viongozi na wajumbe wote wa vyama hivyo na akaunti zao na endapo watabainika kuhusika basi pesa zao zote zitumike kuwalipa wakulima hasara walizowasababishia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.