Ubanguaji wa Korosho kuanza katika kiwanda cha BUCO
Waziri wa Viwanda, Biashara, na Uwekezaji, Mhe. Joseph Kakunda ameliagiza jeshi la wananchi Tanzania kuhakikisha wanafanya tathmini ya haraka katika kiwanda cha kubangua korosho cha BUCO ili ubanguaji uanze.
Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi wa kiwanda hicho, Mhe. Kakunda amesema kuwa kiwanda cha BUCO toka kilipobinafsishwa mwaka 2005 kilifanya kazi kwa mwaka mmoja tu ambapo mpaka sasa kimekuwa kikitumika kama ghala la kuhifadhia mazao ya biashara kazi ambayo ni tofauti na makubaliano ya kimkataba.
“Kiwanda hiki kwa sasa kimeshakabidhiwa kwa jeshi la wananchi ambapo SUMA JKT ndio watakao kuwa wakikiendesha, ni matarajia yangu kuwa watafanya kazi ya tathmini ya hali ya mitambo iliyopo kwa haraka na kuwasilisha mapendekezo kwa wakati ili kiwanda kiweze kufanya kazi”, alisema Mhe. Kakunda.
Mhe. Kakunda ameeleza kuwa serikali kwa sasa inamalengo ya kuhakikisha viwanda vyote vilivyobinafsishwa vinafanya kazi kwa mujibu wa mkataba na si vinginevyo. Hivyo ametoa wito kwa wamiliki wote wa viwanda vilivyobinafsishwa nchini kuhakikisha viwanda vyao vinafanya kazi kwa mujibu wa mkataba kabla ya serikali kufanya maamuzi ya kuvichukua na kuwapa watu wenye uwezo wa kuviendesha.
Aidha, viongozi wa vyama vya ushirika waliagizwa kuandaa taarifa sahihi za wakulima wanaowahudumia zitakazoainisha jina kamili, umri, jinsia, mahali alipo, namba ya akaunti, kiasi cha korosho alichopeleka, ukubwa wa shamba lake na idadi ya mikorosho aliyonayo. Taarifa hii itasaidia sana katika taratibu za malipo pamoja na upangaji wa mipango ya baadae kama ya uagizaji wa pembejeo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi alisema kuwa kiwanda hicho kikianza kufanya kazi kitatoa fursa za ajira, kitaongeza mzunguko wa fedha, na kuongeza wigo wa uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na zao la korosho ambapo wataalam wanasema korosho ina bidhaa takribani kumi na tano.
Pia amewaonya waendesha maghala, watendaji na viongozi wa vyama kutofanya udanganyifu au ukwamishaji wa aina yoyote badala yake wawe ni waaminifu kwa kila mmoja kuhakikisha anatimiza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
"Mameneja wa vyama vikuu hakikisheni wanaolipwa niwale wenye mashamba yanayolingana na korosho walizoleta. Msiwaandikishe watu ambao hawana mashamba, kwani hao ndio watakuwa walionunua kangomba na ikibainika hatua zitachukuliwa dhidi yenu”, aliwaonya Mhe. Zambi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.