Mnada wa kwanza wa ufuta waonyesha mwanga
Mnada wa kwanza wa ufuta umeonyesha mwanga baada ya kilo ya ufuta kununuliwa kwa zaidi ya bei elekezi iliyowekwa na mkoa.
Haya yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake baada ya mnada wa kwanza wa ufuta kufanyika katika Kijiji cha Kitomanga Halmashauri ya Wilaya ya Lindi. Mnada huu umesimamiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao ambacho kinajumuisha wilaya ya Lindi na Kilwa.
Mhe. Zambi alisema kuwa mnada wa kwanza umeonyesha mafanikio kwani kilo moja ya ufuta imenunuliwa kwa sh. 2710 huku jumla ya kilo zilizoingizwa kwenye mnada ni 632,000 na zote zilinunuliwa. Bei elekezi ya ununuzi wa ya ufuta kwa kilo kwa msimu huu 2017/2018 ni sh. 1764 huku makato yakiwa ni sh. 103.
“Mnada huu wa kwanza umeanza vizuri kwa kilo moja ya ufuta kununuliwa kwa sh. 2710, ni matarajio ya mkoa kuwa bei hii itaendelea kupanda kwani kati ya kampuni 19 zilizojitokeza kwa ajili ya kununua ufuta katika mnada wa kwanza ni kampuni mbili tu ndizo zilizofanikiwa kununua ufuta wote ambazo ni Sunshine Commodities iliyonunua kilo 219,000 na The Agro Processing Africa Limited (TAPAL) iliyonunua kilo 413,000”.
“Kwa kuwa Ufuta bado unaendelea kukusanywa katika maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa wa Lindi, niwaombe wakulima kuhakikisha wanauza ufuta wao kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Mkoa na sio kuuza ufuta kwa njia ya chomachoma ili waweze kunufaika na bei nzuri”, alisema Mhe. Zambi.
Aidha, Mhe. Zambi amewataka wananchi kuelewa kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa sio msimamizi wa biashara ya ufuta bali ni msimamizi wa kuhakikisha utaratibu wa ununuzi wa ufuta uliowekwa unatekelezwa. Hivyo msimamizi mkuu wa minada ya uuzwaji wa ufuta ni vyama vikuu vya ushirika ambapo kwa Mkoa wa Lindi kipo Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao na Chama Kikuu cha Ushirika cha RUNALI (kinajumuisha wilaya za Ruangwa, Nachingwe na Liwale).
Pia viongozi katika ngazi zote wametakiwa kuhakikisha wanasimamia mwongozo wa ununuzi wa zao la ufuta uliopitishwa na mkoa, na kuhakikisha wanadhibiti biashara ya chomachoma katika maeneo yao. Katika misimu iliyopita zao la ufuta limekuwa likinunuliwa kwa mfumo ambao sio rasmi tofauti na utaratibu unaotumika katika msimu huu.
Mkoa kwa kushirikiana na Halmashauri uliweka utaratibu wa ununuzi wa ufuta ambapo kampuni yoyote inalazimika kufuuata ili iweze kuwa mnunuzi halali. Utaratibu huu unapatikana katika tovuti ya mkoa eneo la matangazo ambapo pia matangazo mbalimbali ya minada yatakuwa yakitolewa.
Baadhi ya wananchi wa Kitomanga na vijiji jirani
wakishuhudia mnada wa kwanza ukiendeshwa katika kijiji chao.
Vilevile Mhe. Zambi ametumia fursa hiyo kuwajulisha wanalindi kuwa mkoa utapokea Mwenge wa Uhuru Juni 20, 2018 katika Kijiji cha Madangwa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi ambapo utazunguka Halmashauri zote. Juni 26, 2018 Mwenge wa Uhuru utaondokea Halmashauri ya Manispaa katika uwanja wa ndege wa Kikwetu kuelekea Zanzibar. Mhe. Zambi amewasihi wananchi na viongozi wote kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote ambayo Mwenge wa Uhuru utapita na katika maeneo ya mkesha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.